Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Dawati la Jinsia na Watoto

MPANGO KAZI WA TAIFA WA KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO

(MTAKUWWA: 2017/18 – 2021/22)

1. Utangulizi

Usimamizi na utekelezaji wa afua za kutokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto nchini ni miongoni mwa maeneo mtambuka ambapo uhusisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Serikali. Kwa vipindi tofauti kuanzia mwaka 2000 Serikali kwa kushirikiana na Wadau ilikuwa ikitekeleza mipango nane (8) iliyolenga kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ikiwa ni jitihada za kuleta usawa katika jamii.

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika uzuiaji wa vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto na utoaji wa huduma kwa waathirika wa vitendo hivyo, utekelezaji wa mipango hiyo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu katika uratibu na upatikanaji wa taarifa za uhakika za vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto nchini. Aidha, kulikuwa na mwingiliano wa kiutendaji miongoni mwa wadau katika utekelezaji wa afua za kutokomeza ukatili nchini na hivyo kusababisha matumizi ya rasilimali watu na fedha kukosa tija, weledi na uwajibikaji.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali kwa kushirikiana na Wadau ilichukua hatua ya kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA; 2017/18 – 2021/22), ili kuwa na mpango jumuishi kwa madhumuni ya kuboresha utekelezaji wa afua za ulinzi kwa Wanawake na Watoto kwa kuweka mazingira salama na rafiki kwa maendeleo yao.

2. Malengo ya Programu

Programu ya MTAKUWWA inatarajia kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na uratibu wa afua za kutokomeza vitendo vya ukatili nchini ili kuwezesha kufikiwa kwa malengo yaliyoainishwa ya kupunguza aina zote za ukatili nchini kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022. Aidha, Programu inalenga kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo mapungufu katika Eneo la Uratibu na Upatikanaji wa Takwimu za uhakika za vitendo vya ukatili kwa Wanawake na Watoto nchini.

3. Muundo wa Usimamizi wa Programu

 Kwa mujibu wa Mwongozo wa Uratibu wa Programu ya MTAKUWWA, mfumo wa uratibu unaanzia ngazi ya Taifa, Tawala za Mikoa hadi ngazi ya Serikali za Mitaa kama ifuatavyo:- 

 

 -Kamati Elekezi ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto (Kamati ya Makatibu Wakuu);

-Kamati Tendaji ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto (Kamati ya Wakurugenzi);

-Sekretariet ya Kamati Tendaji;

-Vikundi Kazi  vya Utekelezaji wa MTAKUWWA;

-Kamati ya Mkoa ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto;

-Kamati ya Wilaya ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto;

-Kamati ya Kata ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto; na

-Kamati ya Kijiji/Mtaa ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto.  

Kamati hizo zitakuwa na jukumu la kuratibu utekelezaji wa MTAKUWWA katika ngazi husika. Wadau wote wanaotekeleza MTAKUWWA wanalazimika kufanya kazi na Kamati katika ngazi husika na kuhakikisha taarifa zote za shughuli wanazotekeleza zinahuishwa katika taarifa za Kijiji/Mtaa, Kata, Halmashauri, Mkoa na Taifa.

ZINGATIA:

Ofisi ya Rais – TAMISEMI inahusika moja kwa moja na kuratibu shughuli za utekelezaji wa Mpango katika ngazi za Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

4. Jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu

 Kwa mujibu wa MTAKUWWA, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu ndiye Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto ngazi ya Taifa. Kamati hii inalo jukumu la kutoa miongozo ya kisera na kuratibu utekelezaji wa MTAKUWWA pamoja na shughuli za utoaji huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi. Katibu wa kamati ni Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya kusimamia masuala ya Wanawake na Watoto. Aidha, Kamati hii hukutana mara mbili (2) kwa mwaka.