Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

ASDP II

UTANGULIZI

Serikali inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Programu hii ni muendelezo wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Kwanza ambayo ilitekelezwa mwaka 2006/2007 hadi mwaka 2013/2014. ASDP II ni Programu ya miaka kumi iliyoanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 na imepangwa kutekelezwa katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano hadi mwaka 2027/2028.

MALENGO MAKUU YA PROGRAMU

Malengo makuu ya Programu ya ASDP II ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao, usalama wa chakula na lishe.

MAENEO MAKUU YA PROGRAMU

Programu hii ina maeneo makuu manne (4) ya kipaumbele ambayo ni :- (i) Usimamizi Endelevu wa Matumizi ya Maji na Ardhi; lengo likiwa ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji na matumizi bora ya ardhi kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi; (ii) Kuongeza Tija na Faida kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija hasa kwenye mazao ya kipaumbele; (iii)Kuongeza Thamani ya Mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuleta ushindani kwenye soko na sekta binafsi na kuhakikisha uanzishwaji wa vyama vya wakulima; (iv) Kuweka Mazingira Wezeshi ya Kuendeleza Sekta ya kilimo na kuwezesha uratibu, ufuatiliaji na kufanya tathmini ya sekta ikiwa ni pamoja na kuimarisha taasisi na kuweka mazingira wezeshi ya uratibu.

Utekelezaji wa Programu hii unalenga maeneo yote manne ya programu na maeneo ishirini na nne (24) ya kipaumbele ya uwekezaji yenye maeneo ya miradi hamsini na sita (56). Vilevile, fedha za utekelezaji zilikusudiwa kutolewa na Serikali, Wadau wa maendeleo na Sekta binafsi.

URATIBU WA PROGRAMU

Programu inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli wa shughuli za Serikali.

Kwa upande wa Serikali, Programu inatekelezwa na Wizara sita(6) za Msingi ambazo ni Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Wizara za Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Maji, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Vilevile, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Magereza na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia Jeshi la Kujenga Taifa ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa ASDP II upande wa Serikali. Pamoja na hizo pia Wizara ya fedha inahusika ikiwa ni Wizara Wezeshi katika Utekelezaji wa Programu.

UTARATIBU WA VIKAO

Mikutano ya ASDP II katika ngazi ya Taifa inajumuisha Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Sekta ya Kilimo (National Agricultural Sector Stakeholders Meeting-NASSM) ambao utatanguliwa na Mkutano wa Mawaziri wa Wizara za kisekta. Pia kutakuwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Wizara za Sekta ya Kilimo, Kamati ya Usimamizi na Maamuzi ya Sekta ya kilimo (Agricultural Sector Committee - ASC), Kamati ya Ushauri wa Sekta ya Kilimo (Agricultural Sector Consultative Group-ASCG), Kamati ya Ufundi ya Wakurugenzi (Technical Committe of Directors) na mikutano ya Kitengo cha Taifa cha Uratibu wa ASDP II ambacho kitaongozwa na Mratibu mkuu wa Programu.