MRADI WA KUKABILIANA NA VITENDO VYA KIHALIFU KATIKA MAZIWA NA BAHARI KUU NCHINI (TIMA)
1. 0 UTANGULIZI
Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Maziwa na Bahari Kuu nchini "Tackling Illegal Maritime Activities"(TIMA), unatekelezwa na Serikali kupitia ufadhili wa Serikali ya Japan pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Jumla ya gharama za utekelezaji wa mradi huo ni Dola za Kimarekani 900,000. Kati ya kiasi hicho, Dola za Kimarekani 500,000 zitatolewa na Serikali ya Japan na Dola za Kimarekani 400,000 zitatolewa na UNDP.
2.0 MALENGO NA MAENEO MAKUU YA MRADI
Lengo la mradi huu ni kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa. Mapambano hayo yatahusisha kuimarisha juhudi za kupambana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi haramu, uhamiaji haramu, usafirishaji wa madawa ya kulevya, na utoroshwaji wa nyara za Serikali. Maeneo makuu ya mradi ni;
- Uandaaji wa mwongozo wa Kitaifa kwa ajili ya kupambana na uhalifu katika bahari na maziwa. Mwongozo huo utaainisha wajibu wa kila mdau;
- Kuimarisha doria katika bahari kwa kutumia boti itakayonunuliwa na mradi;
- Mafunzo kwa wavuvi wadogo na ujenzi wa miundombinu ya ukaushaji wa samaki; na
- Uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya mradi.
3.0 KAMATI YA USIMAMIZI WA MRADI
Utekelezaji wa mradi utasimamiwa na Kamati ya Usimamizi wa Mradi. Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kuidhinisha Mpango kazi na taarifa za utekelezaji. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Katibu Mkuu (OWM). Wajumbe wengine kwenye Kamati hiyo ni Makatibu Wakuu wa Wizara zifuatazo: TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais, Fedha na Mipango; Mifugo na Uvuvi (Uvuvi); Ulinzi, Mambo ya Ndani, Maliasili na Utalii na Ujenzi na Uchukuzi.
4.0 MANUFAA YA MRADI
Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Uhalifu katika Maziwa na Bahari Nchini una manufaa makubwa kwa Taifa kwa kuwa utasaidia kupunguza uhalifu na kuimarisha ulinzi na usalama katika Maziwa na Bahari.