MPANGO JUMUISHI WA KITAIFA WA MASUALA YA LISHE (NMNAP 2016/17 – 2020/2021)
Ofisi ya Waziri Mkuu kama mratibu wa masuala ya lishe nchini ina wajibu wa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe “National Multasectoral Nutrition Action Plan” (NMNAP). Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Lishe na Mkakati wake wa utekelezaji wa miaka kumi (2015/16 – 2025/26). Mpango umeainisha afua mbalimbali za lishe zinazopaswa kutekelezwa nchini katika kipindi cha miaka mitano (2016/17 – 2020/21). Wizara zinazotekeleza Mpango huu ni pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI; Ofisi ya Waziri Mkuu; Wizara za Fedha na Mipango; Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Kilimo; Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Maji. Aidha, Taasisi ya Chakula na Lishe ndio inayotoa ushauri wa kitaalam katika kusimamia na kutekeleza Mpango huo.
Lengo la Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe (NMNAP 2016/17 – 2020/21) ni kupambana na utapiamlo katika aina zake zote.
3. MUUNDO WA USIMAMIZI WA MPANGO
Utekelezaji wa Mpango unasimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndio Mwenyekiti wa Kamati Elekezi (Katibu Mkuu – Ofisi ya Waziri Mkuu) na Kamati ya Uongozi (Mkurugenzi Idara ya Uratibu). Aidha, Taasisi ya Chakula na Lishe ndio inayotoa ushauri wa kitaalam katika kusimamia na kutekeleza Mpango huo.
4. KAMATI ELEKEZI YA KITAIFA YA LISHE
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu ndiye Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Kitaifa ya Lishe ambayo wajumbe wake ni Makatibu Wakuu wa Wizara tisa zinazotekeleza masuala ya lishe (OR-TAMISEMI, Afya, Elimu, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Maji na Maendeleo ya Jamii). Wajumbe wengine ni wawakilishi kutoka mashirika Umoja wa Mataifa, Washirika wa Maendeleo, Asasi za Kiraia na mtandao wa biashara (business network). Kamati hii ndio yenye wajibu wa kusimamia na kushauri kuhusu masuala yote ya lishe Nchini.