Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wadau wa Afya Moja Wakutana Kuandaa Nyenzo kwa ajili ya Kutoa Elimu Kuhusu Afya Moja


Wadau wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara za Kisekta, Taasisi za Serikali, Shirika la Wanyama Dunia (WOAH), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Afya Duniani (WHO), wamekutana leo tarehe 15 Julai, 2024, Jijini Arusha kwa lengo la kuandaa nyenzo kwa ajili ya kutoa Elimu kuhusu utekelezaji wa dhana ya Afya Moja.

Akizungumza wakati wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi Msaidizi- Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. Salum Manyatta amesema kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.6 ya Mwaka 2022 Ofisi ya Waziri Mkuu inawajibu wa kuratibu wizara, idara, wakala, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na sekta binafsi katika utekelezaji wa mikakati, mipango na miongozo ya dhana ya Afya Moja.

“Utekelezaji wa shughuli zote za Afya Moja zinakwenda vizuri. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utekelezaji wa dhana ya Afya Moja walitengeneza jumbe mahsusi zitakazotumika kuelimisha, kuhabarisha, kuhamashisha, kushawishi na kuimarisha uwezo katika kukabiliana na matukio yenye athari kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira. Tupo hapa kuboresha nyenzo za utoaji elimu kuhusu dhana hii,” amefafanua Dkt. Manyatta.

Afya Moja ni mbinu fungamanishi na jumuishi inayolenga kuhakikisha afya endelevu kwa binadamu, wanyama na mazingira. Utekelezaji wa mbinu hii unatambua uhusiano wa kiikolojia wa afya ya binadamu, wanyama wa kufugwa, wanyama pori, mimea na mazingira. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), utekelezaji wa mbinu hii unawezesha kudhibiti magonjwa kwa uwanda mpana kwa kutambua chanzo, kujiandaa, kukabiliana na ugonjwa mahsusi pindi unapotokea.Aidha, mbinu hii inatekelezwa katika ngazi za kitaifa, kisekta na kijamii, hivyo ufanisi wa utekelezaji wa Afya Moja hutegemea uratibu na usimamizi imara katika ngazi zote za kiutekelezaji.

Zaidi ya hayo, umuhimu wa Afya Moja ni kuongeza ufanisi wa kukabiliana na majanga na maafa yanayohusiana na magonjwa, kusaidia ushirikishanaji wa taarifa na rasilimali katika kudhibiti na kupunguza madhara yatokanayo na majanga na maafa ya magonjwa, na kujenga ustahimilivu wa jamii mbele ya milipuko ya magonjwa, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, usalama wa chakula na lishe, na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

 

=MWISHO=