Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali imetoa trilioni 3.5 kuwawezesha vijana-Majaliwa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imefanikiwa kutoa kiasi cha shilingi trilioni 3.5 kufikia mwaka 2024 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi kutoka shilingi bilioni 904 mwaka 2021.

Amesema kuwa fedha hizo zimewasaidia vijana kupata mitaji ambayo imewawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na hatimaye kuinua vipato vyao pamoja na uchumi wa Taifa.

Amesema hayo leo Ijumaa (Oktoba 10, 2025) wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa iliyofanyika mkoani Mbeya. Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo ni Nguvu Kazi ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imefanya hivyo kwa kutambua kuwa Vijana ni nguvu kazi  na ndiyo msingi wa safari ya maendeleo ya Taifa. “Vijana wakipewa nafasi na kuandaliwa ipasavyo, wanaweza kuwa nguzo kuu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na kufanikishaMalengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs)”.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa vijana wamekuwa nguzo muhimu ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini na wamechangia kwa kiwango kikubwa katika kilimo, biashara, teknolojia, michezo na sanaa. 

“Katika nyanja za ubunifu na teknolojia, vijana ndiyo vinara wa matumizi ya teknolojia mpya na majukwaa ya kidijitali, ikiwemo akili mnemba (artificial intelligence) na mifumo ya mawasiliano ya kisasa, Michango yao imekuwa kichocheo cha mabadiliko chanya katikajamii na uchumi wa Taifa.”

Pia Mheshimiwa ametoa wito kwa wadau wote kuhakikisha vijana wanashirikishwa kikamilifu katika ngazi zote za maamuzi na si tu kama wanufaika wa sera bali pia kama wabunifu na viongozi wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi 

Akizungumza alipotembelea Banda la VETA , Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Taasisi hiyo pamoja wadau wengine wa elimu kuwapa kipaumbele cha mafunzo watu Wenye Ulemavu pamoja na kuwaandalia nyenzo muhimu za kujifunzia ili waweze kutumia ujuzi watakaoupata kuongezea kipato.

“Baada ya kutembelea Banda hili nimejifunza kwamba wapo vijana Wenye Ulemavu wana ujuzi na vipaji, wazazi tuwe tayari kuwaatoa watoto wetu Wenye Ulemavu na Taasisi za elimu ziwapokee na kuwapa ujuzi”

Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kundi la Vijana na ndiyo maana inawekeza na kuthamini mchango na nguvu zao katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii. 

“Hii ni rasilimali kubwa ambayo ikielekezwa na ikijengewa uwezo ipasavyo kupitia vipaji walivyonavyo italeta maendeleo endelevu, kujenga Taifa shindani na lenye ustawi”.