Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Naibu Waziri Ummy Atoa msukumo kwa watumishi kuongeza ufanisi, aagiza utekelezaji thabiti wa bajeti


Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga, amewahimiza watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na weledi ili kuhakikisha malengo yaliyoainishwa katika bajeti ya Serikali yanatekelezwa ipasavyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika leo Jijini Dodoma, Mhe. Ummy—aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. William Lukuvi—alisisitiza umuhimu wa watumishi kushirikiana na kuzingatia misingi ya uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alifafanua kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kufuatia Tamko Na. 1 la mwaka 1970 lililotolewa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, likiwa na lengo la kuongeza ufanisi na tija mahali pa kazi.

“Kupitia mabaraza haya, wafanyakazi na waajiri hupata fursa ya kujadili na kubadilishana mawazo kwa manufaa ya taasisi. Ni matumaini yangu kuwa majadiliano yenu yatajikita katika kuimarisha utendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Mhe. Ummy.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, alimshukuru Waziri wa Nchi pamoja na Naibu Waziri kwa kushiriki katika kikao hicho muhimu cha Baraza la Wafanyakazi.

Aidha, aliwapongeza viongozi hao kwa ushindi walioupata katika Uchaguzi Mkuu na kwa kuendelea kuaminiwa na Mhe. Rais katika kusimamia sekta hiyo nyeti.

Dkt. Yonazi alieleza kuwa kikao hicho kimewakutanisha Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi ili kujadili bajeti ya ofisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kupitia taarifa ya utekelezaji kabla ya kuidhinisha hatua za kuwasilisha bajeti hiyo katika ngazi zinazofuata.