Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wananchi Mkinga wanufaika na uwekezaji katika kilimo cha mwani


Wananchi wa Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wanatarajiwa kunufaika zaidi kiuchumi kupitia uwekezaji wa Serikali katika sekta ya kilimo cha mwani, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya bahari na kuboresha maisha ya jamii za pwani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kaushio jipya na mashine mbili za kisasa za kusaga mwani uliofanyika katika Kijiji cha Kichaka Miba, Wilaya ya Mkinga, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy H. Nderiananga, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha uchumi wa wananchi wa maeneo ya pwani.

Mradi wa Kuimarisha Usalama wa Bahari unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), na unatekelezwa na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) Tawi la Mwanza kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ambapo Lengo lake ni kuimarisha ufuatiliaji na ulinzi wa bahari pamoja na kuongeza thamani ya rasilimali za baharini kwa manufaa ya jamii.

Mhe. Nderiananga amesema kupitia mradi huo, Serikali imenunua boti mbili za doria, kujenga kaushio la kisasa la mwani, kusimika mashine za kusaga mwani na kutoa mafunzo kwa vikundi vya wakulima. Ameongeza kuwa hatua hizo zitaboresha ubora wa mwani, kupanua masoko, kuongeza kipato cha wakulima na kusaidia kuzuia vitendo vya kihalifu baharini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Dkt. Guvenail Mkonoko, amesema kabla ya utekelezaji wa mradi huo wataalamu walifanya tathmini iliyobaini changamoto za mbinu duni za kilimo, ukaushaji usio salama na ukosefu wa miundombinu ya kisasa ya uchakataji.

Naye mwakilishi wa wakulima wa mwani, Bi. Mwamvua Bwebwe, Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kuongeza uzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao na kuboresha kipato chao.