Habari
Waziri Kabudi ahimiza kukamilika kwa ujenzi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu ) Mhe, Prof. Palamagamba Kabudi ametoa wito kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha umaliziaji ujenzi wa Jengo la Ofisi hiyo unakamilika kwa wakati ili kusaidia kuendelea kutoa huduma bora za Ofisi.
Waziri amesema hayo alipotembelea kujionea maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hiyo leo Mtaa wa Kilimani Jijini Dodoma ambapo amepongeza kwa hatua za ujenzi uliofikiwa na kuelekeza Mkandarasi kuhakikisha anamaliza ujenzi wa Jengo hilo kwa wakati.
Waziri amesema, “ujenzi wa Ofisi za Umma lazima ujengwe kwa hadhi na uakisi matarajio ya muda mrefu ujao kulingana na mahitaji ya Ofisi, niwapongeze kwa kuzingatia hilo katika ujenzi wa jengo lenu.”
Kwa upande wake Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Mstaafu Fransis Mutungi amemshukuru Waziri kwa maelekezo aliyotoa, ambapo amesema mipango ya Ofisi ni kuwa na watendaji wa wenye elimu ya siasa, wataalamu wa elimu jamii ambao watasaidi kuchakata na kutoa muongozo kulingana na mambo yanavyokwenda.
“Taasisi hii ni kitovu cha mambo ya siasa tunahitaji wataalamu wenye ujuzi tofauti watakaosaidia katika kufanya tafiti na kutoa taarifa zenye weledi zitakazosaidia taasisi kufanya kazi vizuri zaidi,” alieleza Jaji Mstaafu Mutungi
Awali Mkurugenzi wa Rasilimali Watu Bw,Magohu Zonzo amesema ujenzi wa jengo hilo unatekelezwa na Kampuni ya Group Six Intenational na unasimamiwa na mshauri elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi kupitia kampuni tanzu ya (ARU) kwa ajlili usanifu na usimamizi wa mradi.




