Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Rais Magufuli afuta maadhimisho ya sherehe za Uhuru mwaka huu


 

*Aagiza fedha zilizotengwa zitumike kununulia vifaa vya Hospitali ya Uhuru

RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amefuta maadhimisho ya sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2020 na ameelekeza fedha zilizokuwa zimetengwa kufanikisha sherehe hizo zitumike kununulia vifaa mbalimbali kwa ajili ya Hospitali ya Uhuru.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Alhamisi, Desemba 3, 2020) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dkt. Magufuli ameagiza kiasi cha shilingi milioni 835,498,700 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe za maadhimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara zitumike kwa ununuzi wa vifaa vya hospitali hiyo.

Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) zilizofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Amesema Rais Dkt. Magufuli ameagiza siku hiyo itumike kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii nchini.

Novemba 20, 2018, Rais Dkt. Magufuli aliagiza kiasi cha sh. milioni 995,182,000.00 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru, ambayo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 92.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu inasema: “Miaka 59 ya Uhuru na Miaka 58 ya Jamhuri: Tanzania yenye Uchumi Imara Itajengwa na Watanzania Wenyewe, Tufanye Kazi kwa Bidii, Uwajibikaji na Uadilifu.”

Waziri Mkuu amesema hadi kufikia sasa, ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu shilingi bilioni 4.2. Januari 2019 wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya Simu ya Airtel, Rais Dkt. Magufuli aliagiza kiasi cha shilingi 2,415,151,650.00 zilizotolewa na kampuni hiyo zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo.

-ends-