Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Mkuu wa Wilaya Korogwe Basilla: Elimu ya maafa ipewe kipaumbele


Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Basilla Mwanukuzi ameziasa Kamati za Maafa kuendelea kutoa elimu katika maeneo yao ili kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea na kuweka mkazo katika maafa yanayoathiri maeneo ya Wilaya hiyo.

 Ametoa kauli hiyo tarehe 12 Oktoba, 2022 wakati akifungua semina ya siku 5 ya kujenga uelewa juu ya upunguzaji wa madhara ya maafa katika jamii kwa wajumbe wa Kamati za Maafa Wilaya hiyo iliyohusisha Kata sita zinazoathiriwa na maafa ikiwemo Magoma, Foroforo, Kalalani, Dindira, Bungu na Kizara zilizopo Korongwe mkoani Tanga.

 Semina hiyo iliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IMO) imewafikia zaidi ya wajumbe 50 kutoka katika Kata hizo ikiwemo Viongozi wa dini, Wazee Mashughuli pamoja na Watendaji wa Kata na Vijiji wa Wilaya hiyo.

 Mkuu wa Wilaya aliwaasa wajumbe hao kuendeelea kuwa mabalozi wazuri katika kutoa elimu juu ya kujikinga na madhara yatokanayo na maafa ili kiuendelea kuwa na jamii iliyosalama

 “Yatumieni mafunzo haya kama nyenzo muhimu katika maeneo yenu kuhakikisha mnajilinda na maafa yanayoweza kujitiokeza katika maeneo yenu, kukabili maafa kunahitaji kujitolea kwa mtu mmoja mmoja ili kuwa na mazingira salama,”alisisitiza Mhe. Mwanukuzi

 Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Luteni Kanali Selestine Masalamado akieleza lengo la semina hiyo ni kutoa elimu ya masuala ya maafa kuanzia ngazi ya Halmashauri hadi Kijiji ikiwa ni moja ya jukumu la idara hiyo ili kuwa na uelewa mpana kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa.

 “Idara ya Menejimenti ya maafa imekuwa ikiendesha semina hizo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuendelea kuwajengea uelewa wananchi kuhusu mzingo mzima wa menejimenti ya maafa unaohusisha kuzuia, kujiandaa kukabili, kukabiliana, kurejesha hali pindi maafa yanapotokea katika maeneo yao,”alisema Kanali Masalamado.

Aliongezea kuwa miongoni mwa maeneo yaliyofikiwa ni pamoja  na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwa kuzingatia imekuwa ikikabiliwa na maafa mbalimbali yakiwemo ya uhalibifu wa mazao unaosababishwa na uvamizi wa wanyamapori(tembo), ukame, pamoja na mafuriko.

 Naye Afisa Afya kutoka Wilaya ya Korogwe Bw. Majaliwa Tumaini alieleza mada kuhusu ugonjwa wa ebola aliiasa jamii kuona umuhimu wa kujilinda na kulinda wengine kwa kuzingatia madhara yatokanayo na ugonjwa huu.

“Lazima tuchukue tahadhari zote muhimu kwani ugonjwa huu upo nchi jirani, kila mmoja awe mlinzi wa wenzake huku tukifuatilia maelekezo yanayotolewa na Wizara husika na wataalam wa afya,” alieleza

 

=MWISHO=