Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Tunathamini mchango unaotolewa na wahandisi wanawake


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wahandisi wanawake na kwamba inathamini kazi za kihandisi wanazozifanya katika kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.

Serikali inatambua umuhimu wa tasnia ya uhandisi kwa ustawi wa nchi nzima, hivyo inahitaji kuhamasishwa na kupewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na kutengeneza viongozi wengi zaidi wanawake katika tasnia ya uhandisi. Mheshimiwa Rais amekuwa kielelezo cha ubora, maono, uthabiti na uthubutu kwa viongozi wanawake.”

“Kupitia uongozi wake tumeshuhudia namna anavyoifungua nchi yetu ikiwa ni pamoja na kufungua njia kwa wanawake wengi kuwa na uthubutu na kujiamini. Sasa njia iko wazi kwenu, kazaneni na wekeni bidii ili kazi yenu iendelee kuonekana na Taifa lisonge mbele.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Ijumaa Julai 29, 2022) wakati akizindua Kongamano la Saba la Wahandisi Wanawake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar Es Salaam.

Pia, Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na shughuli mbalimbali ambazo Taasisi ya Wahandisi Tanzania kupitia Kitengo cha Wahandisi Wanawake inajihusisha nazo ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa Serikali katika kufanikisha azma yake ya kuwafikia Watanzania wote kuhusu kupata elimu ya masuala ya kihandisi.

“Ziara mnazofanya kwenye shule za sekondari na vyuo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa kizazi cha baadaye chenye ujuzi na uwezo wa kung’amua mambo mapema kwa maslahi mapana ya ustawi wa nchi. Kitendo hiki pia, ni ishara ya umoja uliopo baina yenu kwani mmeonesha uzalendo mkubwa na kwamba muda wote mnaitakia mema nchi yenu.”

Amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhamasisha wasichana katika shule za sekondari wapende na kusoma masomo ya sayansi na hisabati, kutembelea vyuo vikuu ili kuongea na wanafunzi wa kike wanaochukua kozi zinazohusiana na ujenzi na kuwajengea uwezo wanawake ili waweze kusajili kampuni na kufanya kazi za ukandarasi.

“Niwaase kutumia fursa hii kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika tasnia ya ujenzi. Serikali inatambua mchango wa taaluma ya uhandisi kwa  fani mbalimbali katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia ufanikishaji na ukuaji wa huduma mbalimbali.”

“Kwa takwimu za Machi, 2022 Tanzania ina wahandisi wapatao 30,921 ambapo kati yao wanawake ni 3,982 sawa na asilimia 12.88 tu. Hii ni idadi ndogo sana. Tunahitaji kuwa na wahandisi wanawake wengi zaidi, na hii ikiambatana na ongezeko la mafundi sanifu na mafundi mchundo. Serikali inaunga mkono juhudi hizi kwa kuanzisha shule za sayansi kwa wanawake katika kila mkoa.”

Kwa upande wakeNaibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia sekta ya Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wito kwa wakandarasi na wahandisi washauri wanawake wafanye kazi kwa uadilifu na kuhakikisha miradi inakamilika kama ilivyopangwa na kwa viwango stahiki.

“Nipende kutoa rai kwa Wahandisi Wanawake wote wa fani zote za mlengo wa kihandisi mlioko hapa, muendelee kuhakikisha shughuli za ujenzi zote tunazofanya zinafuata taratibu zote za kihandisi na kuhakikisha thamani ya pesa inaonekana katika miradi yote mnayosimamia na kufanya kazi.”

Mhandisi Kasekenya amesema kwamba hana shaka na wanawake kwani imedhihirika maeneo mengi kuwa wapo makini na wana uwezo wa kufana kazi kwa uaminifu na kwa weledi mkubwa.

Ameongeza kuwa uhandisi kwa wanawake utaongezeka na kuimarika endapo wahandisi

wanawake ambao wako ndani ya tasnia hiyo watashikamana na kufanya kazi kwa bidii na kujitolea kuendesha kampeni za kuwashawishi watoto wa kike wajenge ari ya kupenda masomo ya sayansi na hisabati ambayo ndiyo msingi wa mafunzo ya uhandisi.

Naye, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Said amewashukuru viongozi wakuu wa nchi kwa miongozo wanayoitoa pamoja na kuwaamini wanawake na kuwateua katika nafasi mbalimbali.

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania Mhandisi Rizwan Qadri amesema taasisi hiyo ilianzishwa nchini mwaka 1975 ikiwa na wanachama zaidi ya 4,000 kwa lengo la kukuza fani ya uhandisi ndani na nje ya nchi. Taasisi hiyo ina matawi 16 na imepanga kufungua matawi mengine katika mikoa yote nchini.

Naye, Mwenyekiti Kitengo cha Wanawake, Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Upendo Haule amesema pamoja na mambo mengine, kitengo chao kimefanikiwa kuwahamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi ili waje kuwa wahandisi pamoja na kuwahamasisha wahandisi wanawake kufanya kazi kwa kufuata maadili na kanuni za kihandisi.

Amesema wahandisi wanawake wengi wanauwezo mkubwa wa kufanyakazi, hivyo ameiomba Serikali izidi kuwapa nafasi zaidi ili waendelee kuonesha uwezo wao katika ufanyajikazi na kwamba hawatoiangusha.