Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Mwigulu: Ifikapo 2030 Mwanza-Dodoma kwa SGR


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi, kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), wakandarasi na taasisi zinazohusika na uhamasishaji wa fedha, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya Reli ya Kisasa (SGR), akilenga kuona ifikapo mwaka 2030 wajumbe kutoka Mwanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa wakisafiri kwa treni kutoka Mwanza hadi Dodoma.

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 04, 2026) wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge la 13, Mkutano wa Nne, jijini Dodoma.

“Naziagiza Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi, zikishirikiana na Shirika la Reli, wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga vipande hivi pamoja na wale waliopewa jukumu la kuhamasisha fedha za miradi hiyo, kupambana usiku na mchana,” amesema.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha vipande vya Mwanza–Isaka, Isaka–Tabora, Tabora–Kigoma na Makutupora–Dodoma vinaendelea kutekelezwa kwa kasi.

“Ikiwezekana, ifikapo mwaka 2030, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Mwanza, Mara, Shinyanga, Geita na Kagera waje Dodoma wakiwa wamepanda SGR kutoka Mwanza hadi Dodoma,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameiagiza Wizara ya Madini kuchukua hatua za haraka na kali kwa mujibu wa sheria dhidi ya watu wanaoshikilia leseni nyingi za madini bila kuziendeleza, akieleza kuwa hali hiyo inawanyima Watanzania wengine, hususan vijana na wachimbaji wadogo, fursa ya kufanya shughuli za uchimbaji.

“Mheshimiwa Waziri, futeni leseni hizo kwa mujibu wa sheria na gaweni upya maeneo hayo kwa wawekezaji Watanzania, vijana wa Kitanzania na wachimbaji wadogo,” amesema.

Dkt. Mwigulu amewataka Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, watendaji wa Serikali na halmashauri kuhakikisha wanawasikiliza wananchi, wanatatua kero zao kwa wakati na kutoa mrejesho.

Amesema ziara za viongozi wakuu hazipaswi kuwa mbadala wa utatuzi wa kero za wananchi katika ngazi za kawaida za Serikali.

“Kwa msingi huo, nawaagiza tena watendaji wote wa Serikali kuweka utaratibu wa kuwasikiliza wananchi, kutatua kero zao na kutoa mrejesho,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amezitaka taasisi za Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, ikiwemo gharama za uendeshaji wa magari, safari, mikutano, warsha na makongamano, akisisitiza umuhimu wa kuelekeza fedha kwenye vipaumbele vya maendeleo.

Amesema hatua hiyo ni muhimu hasa kutokana na mahitaji makubwa yanayotarajiwa katika sekta ya elimu kuanzia mwaka 2028.

“Tusipobadili tabia ya matumizi, watoto wetu wanaweza kurudi tena kusomea chini ya miti. Tusirudi huko. Tayari tumeshavuka,” amesema.

Dkt. Mwigulu pia amezitaka Kamati za Maafa kuanzia ngazi ya vijiji hadi taifa kujiandaa kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini kuanzia wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba 2026.

Amesema maeneo hatarishi yanapaswa kutambuliwa mapema, huku vifaa vya uokoaji, huduma za dharura na mifumo ya mawasiliano vikiwa katika hali ya utayari.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote tangu Januari 2026 na amewataka Watanzania wenye uwezo kujiunga ili mfumo huo uweze kuwasaidia pia wananchi wasiokuwa na uwezo.

Amesema Serikali tayari imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 48 kusaidia matibabu ya magonjwa ambayo Watanzania wengi hawawezi kumudu gharama zake.

Kuhusu maandalizi ya AFCON 2027, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja, miundombinu ya usafiri, huduma za maji, umeme na afya, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha Tanzania inanufaika kiuchumi kwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Aidha, amezitaka timu za Tanzania zitakazoshiriki mashindano ya CAF kufanya vizuri na kuwataka Watanzania kuweka mbele uzalendo kwa kuziunga mkono timu zote zinazowakilisha nchi

Baada ya kutoa maelezo hayo, Dkt. Mwigulu ameomba Bunge la 13, Mkutano wa Nne, liahirishwe hadi Jumanne, Oktoba 27, 2026, saa 3:00 kamili asubuhi, litakapokutana tena katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.