Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Mwigulu: Serikali imeweka Sh. bilioni 48 kwenye Bima ya Afya kwa Wote


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema tayari Serikali imeweka zaidi ya sh. bilioni 48 ikiwa ni utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ulioanza Januari, mwaka huu.

“Serikali imeanza utekelezaji wake mwezi Januari mwaka huu, kama ilivyokuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uchaguzi. Serikali tayari imeweka fedha za awali, zaidi ya shilingi bilioni 48 hadi bilioni 50, kwa lengo la kuhakikisha makundi ya awali yanapata huduma hiyo na kuokoa maisha yao. Hatua inayoendelea ni Serikali kutafuta vyanzo vya mapato ili kuongeza wigo wa wanufaika wanaotakiwa kunufaika na bima ya afya kwa wote,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, leo (Alhamisi, Septemba 03, 2026) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Nasriya Nasir Ali, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha upatikanaji wa haraka wa bima ya afya kwa wote kwa wanawake, vijana, watoto na watu wenye ulemavu.

Amewataka Watanzania watofautishe Bima ya Afya na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwani Bima ya afya ni programu inayotakiwa kuwahusisha wananchi wote ili waweze kusaidiana katika kupata huduma za matibabu kupitia mfumo wa bima.

“Tusichanganye Bima ya Afya na TASAF kana kwamba ni mfuko wa kusaidia watu wasiojiweza. La hasha. Tukiibadilisha Bima ya Afya kuwa kama TASAF, tukisubiri Serikali ipeleke fedha ili iwahudumie Watanzania wote, tutakuwa tunajiandaa kuifanya programu hii isitekelezeke vizuri”

“Bima ya afya ni ya wote. Maana yake ni kwamba kila Mtanzania anapaswa kushiriki katika mfumo huu. Kupitia ushiriki huo ndipo tutakapoweza kuwa na bima jumuishi ambayo haitamuacha mtu nyuma, wakiwemo watu wasiojiweza,” amesisitiza.

Amesema kadiri Watanzania wote watakavyohamasika kujiunga na bima ya afya, ndivyo programu hiyo itakavyoweza kutekelezeka. “Kwa hiyo, niwaombe Watanzania na Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuhamasisha wananchi wote kushiriki katika bima ya afya. Serikali itaendelea kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya kusaidia familia ambazo haziwezi kumudu gharama za kujiunga na bima ya afya. 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali iko mbioni kuwalipa maveterani waliopigana vita vya Kagera kwa kuwa sheria ya kuwatambua wazee hao tayari imebadilishwa.

Akijibu swali la Mbunge wa NKasi Kaskazini, Bw. Bazilio Kapunda Mbwilo, Waziri Mkuu amesema ni kweli Serikali ilitoa kauli kuhusu kuwalipa maveterani walioipigania nchi kwa uzalendo mkubwa katika Vita vya Kagera dhidi ya utawala wa Idi Amin na ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulibeba jambo hilo. “Suala hili limekuwepo tangu mwaka 1978/1979 na kwa miaka yote hiyo halikuwa limefikia hatua ya kuwalipa wazee wetu hawa.”

Mbunge huyo alitaka kujua Serikali itaanza lini rasmi kuwalipa maveterani Vita vya Kagera kwa vile muda umepita tangu Serikali ilipotoa kauli ya kuwalipa maveterani hao.

“Nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais imeonekana kwanza kwa kubadilisha sheria ili kuweza kuwatambua wapiganaji wetu walioshiriki katika vita hivyo. Sababu iliyofanya malipo haya kuchelewa kwa muda wote ni kwamba baadhi ya wapiganaji waliokwenda vitani wakati huo hawakuwa wanatambuliwa na sheria zilizokuwa zinawahusu wastaafu wa Jeshi, kutokana na mazingira ya wakati huo,” amesema Waziri Mkuu.

“Sheria tayari imebadilishwa ili kuwatambua wazee wetu hawa. Kilichosalia sasa ni kuoanisha taratibu za malipo. Serikali inatekeleza mambo yaliyo kwenye ahadi na mipango yake, lakini kuna taratibu za malipo zinazosimamiwa na sheria za fedha na bajeti, pamoja na maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,” ameongeza.

Waziri Mkuu amesema taarifa zilizopo zinaonesha kwamba mchakato umefikia hatua nzuri na amelihakikishia Bunge kwamba malipo hayo yataanza kulipwa ndani ya mwaka huu wa fedha.

“Nitumie nafasi hii kuiagiza Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakae pamoja na kuharakisha mchakato huo. Fedha ziliwekwa kwenye bajeti na sheria tayari imebadilishwa. Kwa hiyo, kinachosubiriwa sasa ni kuoanisha taratibu za malipo, na jambo hilo litafanyika. Malipo yataanza ndani ya mwaka huu wa fedha,” amesisitiza.