Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu Kuzindua Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe Awamu ya Pili Tanga


WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano wa Saba wa Wadau wa Lishe utakaofanyika Jijini Tanga hii leo Novemba 18, 2021.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokutana na waandishi wa habari Jijini Tanga ili kueleza maandalizi pamoja na Uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Pili wa Masuala ya Lishe kwa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 pamoja na Mkakati wa Ufuatiliaji Rasilimali.

Lengo kuu la mkutano huu ni kuleta wadau pamoja ili kujadili na kutathmini maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Lishe kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita 2016/17 – 2020/21 pamoja na kujadili vikwazo katika utekelezaji wa afua za lishe, ufanisi wa mipango na bajeti za lishe, ushiriki na ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika utekelezaji, pamoja na kushirikishana uzoefu na mbinu bora za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa masuala ya lishe nchini.

Mkutano wa Saba wa Mpango Jumuishi wa Pili wa Lishe Kitaifa umebebwa na Kaulimbiu ya isemayo; Lishe bora ni msingi wa maendeleo ya rasilimali watu katika uchumi shindani”.

Akitaja mafanikio ya mpango wa awamu ya kwanza alisema mpango jumuishi wa kwanza wa lishe umefanikiwa Kwa asilimia 80 ya malengo waliojiwekea na viashiria kuleta matokeo chanya.

“Kwa ujumla katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Lishe I, asilimia 80 ya malengo na shabaha zimefikiwa kwa mujibu wa viashiria vya matokeo (impact level targets). Mathalani, Udumavu (Utapiamlo wa muda mrefu) kitaifa kiwango kimepungua kutoka asilimia 34.7 mwaka 2014 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018. Ukondefu (Utapiamlo Mkali na wa Kadiri) kiwango cha kitaifa kimeendelea kushuka kutoka asilimia 3.8 hadi asilimia 3.5; Utoaji wa huduma za lishe katika vituo vya kutolea huduma na ngazi ya jamii imeimarika; na Kuimarika kwa uratibu katika ngazi ya Serikali kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,”alisisitiza.

Aidha waziri alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watendaji wanaohusika na afua za  lishe nchini kusimamia vema taratibu za upatikana na ulaji wa lishe bora ili kujenga Taifa imara na lenye nguvu.

Aliongezea kuwa, suala la lishe linatakiwa kupewa kipaumbele kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa lengo likiwa ni kutoa makuzi bora ili kuepuka udumavu.

“Ndugu zangu watanzania napenda kuwakumbusha kwamba Lishe ni msingi wa maendeleo, lishe bora hutoa uhakika wa nguvu kazi imara katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla na bila kuwa na nguvu kazi yenye lishe na afya bora hatuwezi kufanikiwa, pia tutakuwa tunahatarisha jitihada za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda,”alisema Waziri Mhagama.

=MWISHO=