Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Mwigulu ataka Taasisi, Wizara, Mashirika ya Umma kuacha matumizi yasiyo ya lazıma


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa, Taasisi na Mashirika ya Umma nchini ziachane na matumizi yasiyo ya lazima ili kuokoa fedha zitakazoiwezesha Serikali kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo hususan ile iliyosimama kutokana na ukosefu wa fedha za awali kwa wakandarasi.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametaja baadhi ya matumizi yasiyokuwa ya lazima yakiwemo ununuzi wa magari mapya wakati yaliyopo yanaweza kuendelea kutoa huduma, kuchapisha kalenda na kununua vifurushi vya zawadi. “Tunakazi ya kufanya kuhakikisha malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha maisha ya Watanzania yanatimia.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Januari 23, 2026 wakati akizungumza na wananchi baada ya kuzindua Meli ya Mv New Mwanza kwenye bandari ya Mwanza South ambapo amesisitiza watendaji wa taasisi hizo waache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake fedha nyingi zielekezwe katika kukamilisha miradi ya maendeleo.

Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Wizara za kisekta kufanya tathmini ya haraka ya miradi yote yenye wakandarasi ambao hawajalipwa fedha za awali, ili Serikali iweze kuzipatia rasilimali na kuongeza kasi ya utekelezaji wake, hivyo ameelekeza kupitiwa upya kwa matumizi yote yasiyo ya msingi, akisisitiza kuwa mafungu ya ulinzi, usalama na afya yasiguswe.

“Fedha ndogo ndogo tunazozitumia kwa mazoea ndizo zinaweza kumaliza miradi iliyosimama. Ni lazima tubadilishe mtazamo na kuweka kipaumbele kwenye mahitaji halisi ya wananchi. Na kubana matumizi ni sehemu ya uwajibikaji wa viongozi wa umma, lengo la Serikali ni kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.”

Naye, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, mradi wa ujenzi wa meli hiyo  ulikuwa umefikia asilimia 40, huku mkandarasi akiwa amelipwa shilingi bilioni 40.64. “Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imewezesha mradi huu kukamilika kwa kutoa kiasi chote cha fedha kilichosalia.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) Eric Hamisi amesema Meli ya New Mv Mwanza ambayo ni ya kwanza kwa ukubwa katika Ukanda wa Maziwa na Barani Afrika na inawezo wa kubeba abiria 12,000, mizigo tani 400, magari madogo 20 na makubwa matatu na inasafiri kwa muda wa saa 6 hadi 7 kutoka Mwanza kwenda Bukoba.

Mkurugenzi huyo amesema meli hiyo yenye urefu wa mita 92.6 na upana wa mita 17 ina madaraja sita ambayo ni kama ifuatavyo la uchumi lenye uwezo wa kuchukua abiria 834, la biashara watu 200, la pili watu 100, la kwanza watu 60, la juu watu wanne na la watu mashughuri abiria wawili. Mradi huo umegarimu shilingi bilioni 120.56.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumzia kuhusu miradi hiyo ukiwemo wa kituo cha Kikanda cha Kuratibu Uokoaji Majini katika Ziwa Victoria alisema ni faraja kwa wanaMwanza kwa kuwa unawahakikishia usalama wawapo majini.

Kuhusu mradi wa  ujenzi wa Matenki, Vituo vya Kusukuma Maji ya Mabomba amesema ni muhimu kwa wananchi kwani unakwenda kutatua changamoto ya maji katika jiji hilo.

Kadhalima kiongozi huyo ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa Meli ya MV New Mwanza ni mkombozi kwa wananchi hao ambao awali walikuwa wakipata ya usafiri kutokana na uchache wa vyombo vya usafiri.

Awali, Waziri Mmkuu alitembelea mradi wa kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokozi cha Kikanda pamoja na boti ya kubebea wagonjwa ziwa Victoria na boti mbili za uokoaji ambapo amewataka watendaji wa kituo hicho kilichogharimu shilingi bilioni 19.8, kuhakikisha kinaendeshwa kwa saa 24 na kwa ufanisi wa hali ya juu.

Pia, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Kusukuma na Kuhifadhi Maji katika mkoa wa Mwanza, akisisitiza umuhimu wa miradi ya maendeleo katika kuhakikisha maisha bora kwa wananchi.