Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu aagiza kodi na tozo za Mkonge zifanyiwe mapitio


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ifanye mapitio ya kodi na tozo zote za zao la mkonge ili kubaini ni zipi zenye manufaa kwa wadau na Taifa na zile zisizo na tija zifanyiwe utaratibu wa kuondolewa.

Pia, Waziri Mkuu amezitaka taasisi za kifedha nchini zipitie upya kiasi cha riba kinachotozwa kwa wakulima wanaokopeshwa ili zisisababishe wahusika kushindwa kukopa kutokana na ukubwa wa riba.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo jana (Jumatano, Januari 20, 2021) wakati wa kikao chake na wadau wa mkonge kwenye ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga, ambapo alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kufuatilia mwenendo wa mazao yote ya biashara. 

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha zao la mkonge linarudi katika nafasi yake na aliiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kuratibu maendeleo yake kuanzia hatua za utayarishaji mashamba hadi mwenendo wa masoko.

“Mkonge una faida nyingi lakini sisi tumekuwa tunafanya utengenezaji wa nyuzi tu, tutumie wataalamu wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti kwa ajili ya kutumia fursa nyingine zinazopatikana katika zao hili kwa kutengeneza sukari, mbolea na vinywaji.”

Waziri Mkuu alisema Wizara ya Kilimo inapaswa iendelee kukiboresha Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) cha Mlingano na ijiridhishe kama kina vifaa vya kutosha kuzalisha miche ya mkonge. Pia aliiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania ishirikiane kikamilifu na kituo hicho ili kuendelea kuboresha zao hilo.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote zinazolima mkonge nchini pamoja na uongozi wa Bodi ya Mkonge zianzishe kanzidata ili wawe na takwimu za wakulima wadogo, wa kati na wakubwa huku wakianisha ukubwa wa mashamba yao.

Alisema kanzidata hiyo itawasaidia kuwafikia wakulima kwa urahisi pale wanapotaka kutoa elimu kuhusu namna bora ya kulima zao hilo kuanzia hatua za uandaaji wa shamba, matumizi ya pembejeo na upatikanaji wa masoko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Bw. Hussein Bashe alisema mwaka 2020 uzalishaji wa mkonge nchini ulikuwa tani 36,298, malengo yalikuwa ni kuzalisha tani 42,286. Katika kipindi cha 2020-2025, Bodi ya Mkonge ina mpango wa kuongeza uzalishaji na kufikia tani 120,000 kwa mwaka.

Alisema Wizara ya Kilimo itahakikisha nchi inapunguza uagizaji wa magunia ya katani kutoka nje ya nchi ili kuliongezea tija zao. “Kwa kuanzia, katika zao la korosho msimu huu wakati wa kutangaza ‘tender’ ya vifungashio tumeeleza kwamba tunatoa kipaumbele kwa vivungashio vya katani vinavyozalishwa nchini.”

Kufuatia hatua hiyo, alivitaka viwanda vyote vya Serikali vya kutengeneza vifungashio kwa kutumia katani vilivyopewa wawekezaji binafsi vihakikishe vinafanya kazi kwani Wizara ya Kilimo haitasita kushauri Serikali ivirudishe Serikalini vile ambavyo havitafanya kazi kufikia mwishoni mwa mwaka fedha wa 2020/2021.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Bw. Saddy Kambona alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020, kampuni ya mkonge ya Amboni Plantation iliongoza kwa upande wa wakulima wakubwa kwa kuzalisha tani 8,277 katika shamba la hekta 14,000 ikifuatiwa na kampuni ya Melt iliyozalisha tani 4,922.53 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 33,000 huku wakulima wadogo nchini wakiongoza kwa kuzalisha tani 9,728.63.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuhakikisha zao hilo linafufuliwa na tayari imefanya utafiti wa kutosha ambapo inatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.