Habari
Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa yaidhinisha mpango wa dharura wa taifa wa kukabiliana na madhara ya el niƱo
Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu ya Usimamizi wa Maafa imeidhinisha Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Niño na kuzielekeza Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri kuongeza kasi ya maandalizi ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotabiriwa kudumu hadi mwisho wa mwaka 2026.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, ameelekeza kila sekta kutenga rasilimali zitakazowezesha hatua za kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali katika eneo lake na pia kuandaa mipango ya dharura ya manunuzi. Pia amesisitiza umuhimu wa kutambua mapema maeneo hatarishi, kufanya tathmini za vihatarishi na kuwahamasisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuhamia maeneo salama.
Aidha, Dkt. Yonazi ameelekeza wananchi kupewa elimu kuhusu namna ya kupunguza madhara ya mvua hizo kwa kuweka akiba ya chakula, kulima mazao yanayostahimili mvua nyingi na kutumia fursa zitokanazo na mvua katika kilimo, uvunaji wa maji, ufugaji na uvuvi. Vilevile, amezitaka taasisi husika kuandaa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, mifugo na mimea.
Kamati hiyo pia imeagiza ukaguzi na uboreshaji wa miundombinu muhimu ikiwemo barabara, maji na umeme, kuimarisha usimamizi wa mazingira, kuhakikisha vifaa vya uokoaji, huduma za dharura na mifumo ya mawasiliano vinakuwa tayari wakati wote, pamoja na kuhuisha mipango ya utekelezaji katika maeneo hatarishi.
Aidha, Wizara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zimeelekezwa kufuatilia kwa karibu utabiri na maelekezo ya kitaalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili hatua zote za maandalizi na kukabiliana na athari za El Niño zichukuliwe kwa wakati.
=MWISHO=




