Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Ujenzi wa uwanja mpya Arusha wafikia asilimia 51


Mkurugenzi wa Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bw. Paul T. Sangawe, amefanya ziara ya ukaguzi katika uwanja wa mpira unaojengwa mkoani Arusha, ambapo ametoa wito kwa wananchi kuelimishwa kuhusu maendeleo ya mradi huo pamoja na fursa zinazotokana nao.

Akiwa katika eneo la mradi, Bw. Sangawe alipokea taarifa rasmi ya utekelezaji wa ujenzi huo, ambao kwa sasa umefikia asilimia 51 ya kazi zote, kiwango kinachozidi malengo ya mpango kazi wa asilimia 50 kwa kipindi hiki. 

Ziara hiyo ilifanyika Mkoa wa Arusha, ambapo mradi huo unatekelezwa kama sehemu ya miradi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Taarifa ya maendeleo ya mradi ilitolewa na msimamizi wa mradi, Bw. Ruta Chakupewa, ambaye alieleza hatua zilizofikiwa na kazi zinazoendelea.

Mradi huu, unaotarajiwa kumalizika kwa wakati, unalenga kuongeza miundombinu ya michezo nchini na unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000. Kazi zinazoendelea ni pamoja na Ukamilishaji wa majukwaa, Ujenzi wa vyumba mbalimbali katika sakafu ya chini, Ufungaji wa miundombinu ya umeme, zimamoto, na TEHAMA 

Bw. Sangawe alisisitiza umuhimu wa kuwaeleza wananchi juu ya kazi zinazoendelea na kuhamasisha uelewa juu ya fursa za kiuchumi, ajira, na maendeleo ya Jamii zinazotokana na miradi kama hiyo

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha uwazi na ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa manufaa ya Watanzania.