Habari
Rais Dkt. Samia Azindua rasmi majengo ya ofisi na miundombinu ya kisasa Mji wa Serikali Mtumba, asisitiza kusogeza huduma karibu na wananchi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Majengo, Barabara na Miundombinu ya kisasa katika Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma, tarehe 30 Oktoba, 2026.
Akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi waliohudhuria hafla hiyo ya kihistoria, Mhe. Rais amesema kuwa kuzinduliwa kwa Mji wa Serikali Mtumba ni mafanikio makubwa katika mpango wa kuhamishia makao makuu ya serikali na kusogeza huduma muhimu karibu zaidi na wananchi.
Katika uzinduzi huo Mhe. Dkt. Samia ameambatana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço ambapo amekata utepe katika jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kuashiria ufunguzi wa majengo yote ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali yaliyojengwa katika mji huo.
Amesema kukamilika kwa majengo hayo hakumaanishi wananchi wote wanapaswa kusafiri hadi Mtumba kupata huduma, bali taasisi za Serikali zinapaswa kutumia mifumo ya TEHAMA kurahisisha utoaji wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesisitiza umuhimu wa mifumo ya TEHAMA inayotumiwa na taasisi za Serikali kuweza kubadilishana taarifa ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kuwasilisha taarifa zilezile katika ofisi tofauti.
“Nitoe rai kwenu Watendaji wa Serikali kwamba, pamoja na huduma za Serikali kupatikana hapa Mji wetu wa Serikali Mtumba, bado wananchi hawapaswi kulazimika kuja hapa makao makuu ya nchi kufuatilia kila huduma inayotolewa na Serikali.” Amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.
=MWISHO=




