Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Mkataba wa Ujenzi wa Meli Tatu za Uvuvi wa Bahari Kuu Wasainiwa


Serikali kupitia Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) imesaini mkataba wa ujenzi wa meli tatu za uvuvi wa bahari kuu na Kampuni ya Rongcheng Xinyang Ship Industry Limited ya China, ikiwa ni hatua ya kuimarisha na kuongeza tija katika sekta ya uvuvi nchini.

Mkataba huo umesainiwa leo, Agosti 24, 2026,Jijini Dar es Salaam kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ambapo Shirika la Uvuvi Tanzania - TAFICO  kuwa na meli mbili Kwa upande wa Tanzania bara na Shirika la Uvuvi Zanzibar -ZAFICO kuwa na meli moja.

Akizungumza wakati wa kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Kakurwa, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya uvuvi.

Dkt. Kakurwa ameishukuru IFAD kwa ufadhili wa ujenzi wa meli hizo kupitia AFDP, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kufungua fursa zaidi za uvuvi wa bahari kuu na kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, amesema Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa Mratibu Mkuu wa AFDP, inatambua utiaji saini wa mkataba huo kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa programu hiyo.

Amesema ujenzi wa meli hizo ni hatua itakayochangia ukuzaji wa uchumi kupitia uvuvi wa bahari kuu, pamoja na kuongeza uwezo wa Tanzania kutumia kikamilifu rasilimali zake za bahari.

Naye Mratibu wa AFDP kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Salum Mwinjaka, amesema utiaji saini wa mkataba huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha malengo ya programu yanafikiwa kwa wakati na utekelezaji wake unakuwa na mafanikio.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha walengwa wa programu pamoja na Taifa kwa ujumla wananufaika na fursa zinazotokana na utekelezaji wa AFDP.

AFDP inalenga kukuza uzalishaji endelevu wa kibiashara unaozingatia mazingira, hususan katika uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo kama mahindi, alizeti, maharagwe na jamii ya mikunde, pamoja na uvuvi na ufugaji wa viumbe maji.

Programu hiyo pia inalenga kuwawezesha wanawake na kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji.

AFDP inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na kutekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar kupitia taasisi mbalimbali, ikiwemo TAFICO, ZAFICO, Wakala wa Mbegu (ASA), TARI na TOSCI.

Hatua hiyo ya kusaini mkataba wa ujenzi wa meli tatu inatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania katika uvuvi wa bahari kuu, kuchochea uwekezaji, kuongeza ajira na mapato, na hatimaye kuimarisha mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa Taifa.