Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa atoa rai viongozi wa dini waendelee kuombea amani Tanzania


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wa dini hawana budi kuendelea kuiombea amani Tanzania pamoja na viongozi wake kwani bila amani hata kusanyiko la kidini haliwezi kufanyika.

Akinukuu Quran tukufu sura ya 2, aya ya 126 (Quran 2:126), Waziri Mkuu amesema nabii Ibrahim aliuombea mji wake na wakazi wake amani na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.  “Nami nitoe rai kwa viongozi wetu wa dini, waendelea kuiombea nchi yetu na viongozi wake ili waendelee kuliongoza vema Taifa letu ikiwa ni pamoja na kujenga umoja na mshikamano, kudumisha amani na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.”

Ametoa wito huo leo (Jumapili, Agosti 14, 2022) kabla ya kukabidhi tuzo kwa washindi wa kuhifadhi Quran barani Afrika katika mashindano yaliyofanyika kwenye msikiti wa Mfalme Mohammed VI, ulioko Kinondoni makao makuu ya BAKWATA, jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yamefadhiliwa na Taasisi ya Mfalme wa Morocco Ulamaa Afrika.

Akizungumza kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema kusanyiko la mashindano hayo ni kielelezo cha utukufu wa Quran barani Afrika kwani limejumuisha washiriki 88 kutoka nchi 34 barani Afrika.

Amesema katika zama hizi dunia inashuhudia kuongezeka kwa vitendo viovu ikiwemo watoto kuuwa wazazi wao; ulawiti; ubakaji hususani kwa watoto na wanafunzi; watoto na vijana kutowaheshimu watu wazima; uvaaji wa mavazi yasiyo na stara hususani kwa wasichana na wavulana na matumizi ya madawa ya kulevya. 

“Tunapaswa kutambua kuwa tupo katika zama zinazokabiliwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa rika zote. Ni jambo zuri, jambo bora na jambo tukufu kabisa kukaa, kuisoma na kuisikiliza Quran. Lakini swali la msingi ni kwa kiasi gani tunaizingatia hii Quran katika mwenendo mzima wa maisha yetu ya kila siku. Kwa lugha nyingine, tunapowahifadhisha Quran vijana wetu tuhakikishe jambo hilo jema linakwenda sambamba na ujenzi wa misingi imara katika kujenga jamii bora,” amesema.

Amesema Quran inapaswa kuwa chanzo cha kutegemewa cha mafunzo sahihi ya tabia njema, utii na kuheshimu mamlaka zilizopo. “Tukiwalea vijana wetu katika mafunzo haya tutakuwa tunamsaidia mlezi wetu namba moja Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaguswa na suala zima la maadili hususan kwa vijana kuwa na wasaidizi wacha Mungu na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao.”

Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini wahakikishe kuwa vijana wanaweza kuhifadhi Quran lakini pia wawe wamehitimu katika fani mbalimbali. “Kijana akihitimu fani yake siyo rahisi kumuona akienda kinyume na maadili ya taaluma yake. Kwa hiyo, Quran ni mchunga wa nafsi ya mtaalamu huyo na hivyo, kumfanya aonyeke dhidi ya kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na uadilifu.“

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo ya kutoa tuzo kwa washindi, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir alimshukuru Mfalme wa VI wa Morocco na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mfalme wa Morocco Ulamaa Afrika, Bw. Mohammed Rifqiy kwa kuamua kuleta mashindano hayo Afrika Mashariki.

“Uamuzi wao wa kuleta mashindano haya umetuwezesha kuona jinsi Quran ilivyokuwa inaandikwa kwa mkono hadi kufikia hatua ya sasa ya kuchapisha. Wenzetu wa Afrika Magharibi wamezoea kuyaona haya.” 

Miongoni mwa washindi waliotia fora ni binti wa miaka 14, Saima Hassan Suleiman wa Dar es Salaam ambaye aliibuka mshindi wa tatu katika kundi la pili la kuhifadhi msahafu kwa riwaya zilizobaki. Yeye alihifadhi juzuu 30.

Saima ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Shaaban Robert ya jijini Dar es Salaam, alisema amekuwa akijifunza Quran tangu akiwa na miaka mitano. Mshindi wa kwanza wa kundi hilo ametoka Niger na wa pili ametoka Gambia.

Mshindi wa kwanza katika kundi la kwanza la kusoma na kuhifadhi Quran kwa mtindo wa riwaya ya warshi (Riwayat Warsh) ni Murtado Olatunji Katibi wa Nigeria. Wa pili ni Abdinassir Hassan Ibrahim kutoka Somalia na wa tatu ni Khatry Dakhay kutoka Mauritania.

Katika kundi la tatu ambalo ni la tajwid, mshindi wa kwanza alikuwa ni Ustaadh Ahmad Salim Mbwewa ambaye ni mwalimu wa watoto jijini Dar es Salaam.