Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa atoa maagizo upatikanaji wa dawa kwa wananchi


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wahakikishe wananchi wanapata dawa wanapokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa sababu Serikali inatoa fedha za kutosha kwa ajili ya huduma hiyo.

”Sitarajii kusikia mwananchi anakwenda kwenye kituo cha kutolea huduma za afya na kukosa dawa kwa sababu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri simamieni suala hilo.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Mei 18, 2025) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua ujenzi wa Akademi ya Michezo katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, hivyo ni jikumu la viongozi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Serikali imefanikiwa kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi mkoni humo, hivyo watahakikisha wanaendelea kuipa ushirikiano Serikali yao.

Mkuu huyo wa mkoa amesema miradi inayoendelea kutekeleza katika mkoa huo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, reli ya SGR, kukamilika kwa daraja la Kigongo-Busisi, meli ambayo yote ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Seikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.