Habari
Kanisa la PAG lakabidhi maguni 40 ya mahindi Hanang’
Kanisa la Pentecostal Assemblies of God (PAG) wilaya ya Hanang' limetoa msaada wa magunia 40 ya mahindi kwa ajili ya waathiriwa wa maporomoko ya udongo, mawe na miti yaliyotokea jumapili Disemba 3,2023 na kuathiri kata nne wilayani humo.
Muangalizi wa makanisa ya PAG wilaya ya Hanang' Mchungaji Philipo Siasi amesema wamekabidhi chakula hicho kuiunga mkono Serikali kufuatia majanga yaliyotokea.
Aidha Mchungaji Siasi amewasihi watu wengine wenye mapenzi mema kuendelea kujitolea huku wale wenye ndugu zao na wenye uwezo wa kuwahifadhi ni vyema kufanya hivyo lengo ni kuendelea kuwasaidia wakati Serikali ikiendelea na hatua za urejeshaji wa hali.
Akipokea misaada hiyo leo Disemba 13, 2023 Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na uratibu Dkt Jim Yonazi amesema Kitendo kilichofanywa na Kanisa hilo kinawatia moyo waathirika wa maafa hayo na serikali.
Mbunge wa Jimbo la Hanang' Mhandishi Samwel Hayuma ameishukuru serikali na wadau wote wanaoendelea kutoa faraja kwa misaada mbalimbali wanayoitoa.
AWALI
Mbali na hivyo Mchungaji Siasi ameongoza maombi maalum kwa ajili ya kuiombea nchi ya Tanzania, Mungu ailinde na kuiepusha na majanga.
Hadi sasa miili iliyopatikana kufuatia maporomoko ya tope, mawe na magogo imefika 89.
=MWISHO=