Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria yatembelea Kiwanda cha Kuchakata Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imewataka wawekezaji na wafanyakazi wa kiwanda cha kimataifa cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro Leather International Co. Ltd (KLICL) kufanya kazi kwa juhudi, weledi na maarifa ili makusudio ya kuanzishwa kwake yafikiwe na kuleta manufaa kwa watanzania.

Hayo yalisemwa Oktoba 23, 2021 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Najma Giga wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo aliwataka watumishi wa kiwanda hicho kuwa wabunifu na waaminifu katika kulinda miundombinu ya kiwanda ili kiendelee kuzalisha bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya watanzania wote na kukabili soko la ushindani ndani nan je ya nchi.

“Kamati itaendelea kusimamia na kushauri uongozi wa kiwanda ili kiwe endelevu na kilete tija nchini na ni jambo la faraja kuwa na kiwanda kama hiki kwa sababu mpango wa Serikali umejidhatiti katika kufufua viwanda ili tuwe na bidhaa zetu za ndani na zitakazokuwa na ubora wa kuuzika katika soko la nje,” alisema Mhe. Gigga

Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.  Patrobas Katambi alishukuru kamati hiyo kwa kutembelea kiwanda hicho na kusema hoja zote zilizotolewa na wajumbe zimepokelewa na zitafanyiwa kazi vyema huku akisisitiza kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha inawajengea uwezo vijana kupitia fursa mbalimbali za miradi mikubwa iliyopo nchini.

“Kiwanda hiki kimefanikiwa kukuza ujuzi kwa vijana na mmeshuhudia pale kwenye mashine asilimia 80 ya wafanyakazi ni vijana na wanajifunza kutengeneza soli za viatu, mikanda, mikoba ya kina mama na bidhaa nyingine za ngozi,” alieleza

Hata hivyo aliwasisitiza watazania kuthamini na kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi badala ya kuagiza bidhaa kutoka nje akisema bidhaa zinazotengenezwa nchini zina viwango vyenye ubora huku akihimiza vijana kutumia fursa za uanzishwaji wa viwanda kupata ajira.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba alisema hadi kukamilika mradi huo utagharimu zaidi ya Bilioni 126.19.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda, Mhandisi Masud Omari alisema kiwanda kimeanza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za ngozi imara na zenye ubora.

“Tumeanza uzalishaji, hivyo tunatoa wito kwa watanzania wote kuvaa viatu vya kiwanda chetu, kwani ni bora na imara na vinapatikana kwa bei nafuu” alisisitiza Mhandisi Omari.

Katika hatua nyingine wajumbe wa kamati wamepongeza mipango ya kiwanda hicho na kushauri kilenge kuwa na viwango vya kimataifa na kutoa ajira kwa watanzania wengi ikiwemo vijana na wanawake na kushauri elimu zaidi itolewe kuhusu bidhaa za kiwanda hicho na maduka yasambae nchi nzima.

Aidha Mbuge wa Moshi Mjini, Mhe. Priscus Tarimo alisema wakazi wa Moshi wapo tayari kulinda kiwanda akisisitiza kuzingatiwa kwa sheria ya udhibiti wa uinizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kuepuka bidhaa feki.