Habari
Dkt. Mwigulu: Tunataka kuwa miongoni mwa wazalishaji 10 bora wa chakula duniani
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania inalenga kuwa miongoni mwa wazalishaji 10 bora wa chakula duniani kutokana na uwekezaji ambao umefanyika kwenye sekta ya kilimo.
“Matarajio yetu ya muda mrefu yameelezwa katika Dira ya Maendeleo Tanzania ya 2050. Chini ya lengo la kwanza, Tanzania inalenga kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika na miongoni mwa wazalishaji 10 bora wa chakula duniani,” alisema.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Alhamisi, Oktoba 22, 2026) wakati akitoa mada kuu kwenye mjadala kuhusu Mustakabali wa Kilimo barani Afrika katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue) unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Iowa, jijini Des Moines, Marekani.
Aliwaeleza washiriki wa mkutano kwamba chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali iliongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 294 za Tanzania kwa mwaka 2021/2022 hadi shilingi trilioni 1.241 katika mwaka 2025/2026. “Hii inadhihirisha jinsi sekta ya kilimo ilivyopewa kipaumbele kama injini ya mabadiliko ya kiuchumi, utengenezaji wa ajira, usalama wa chakula na lishe, ukuaji wa viwanda na mauzo ya nje.”
Kutokana na jitihada hizo, Waziri Mkuu alisema Tanzania imefanikiwa kufikia kuwa na utoshelevu wa chakula wa asilimia 130. “Hii inaonesha uwezo wetu kukidhi mahitaji ya kitaifa ya chakula unaongezeka na kuweza kuzalisha ziada kwa masoko ya kikanda na kimataifa,” alisema na kuongeza: “Mauzo yetu ya nje ya kilimo yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2021/2022 hadi kufikia dola bilioni 3.7 mwaka 2024/2025.”
Alisema nchini Tanzania, kilimo kinabaki kuwa nguzo ya mageuzi ya kiuchumi kwa kuwa hivi sasa inachangia asilimia 24.6 ya Pato la Taifa, inaajiri asilimia 65 ya nguvu kazi na inazalisha takriban asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje na malighafi kwa viwanda nchini.
Alitumia fursa hiyo kumpongeza Mshindi wa Tuzo ya Chakula Duniani wa mwaka 2026 Prof. Huub Lelieveld kwa mafanikio aliyopata akisema kwamba yanaikumbusha dunia kuwa usalama wa chakula haupatikani tu wakati chakula kinapopatikana. “Ukweli wa kisayansi ni kwamba chakula ni lazima pia kiwe salama, chenye lishe na kinachoweza kupatikana kwa bei nafuu.
Prof. Lelieveld ni mwanasayansi wa Uholanzi ambaye amekuwa akijihusisha na masuala ya usalama wa chakula. Ametangazwa kuwa mshindi wa mwaka 2026 na Taasisi ya Tuzo ya Chakula Duniani (World Food Prize Foundation).
Akizungumzia kaulimbiu ya mjadala huo isemayo “Kabla Njaa Haijatushinda”, Waziri Mkuu alisema inahitaji uharaka, lakini uharaka lazima uambatane na matumaini. “Afrika siyo tu bara linalokabiliwa na changamoto za usalama wa chakula bali pia ina uwezo mkubwa wa kuwa mchangiaji mkubwa wa usalama wa chakula duniani. Na Tanzania inakusudia kuwa sehemu ya mabadiliko hayo,” alisisitiza.
“Acha tuwekeze kwa wakulima, na tuwekeze pia katika sayansi. Tuwekeze kwa vijana na wanawake. Tuwekeze katika mifumo thabiti ya chakula. Na zaidi ya yote, tuwekeze katika uwezo wa kilimo barani Afrika. Kwa kweli, kabla ya njaa haijatushinda, tuchukue hatua, tuwekeze na tuvumbue pamoja. Tujenge mifumo ya chakula inayoweza kulisha vizazi vya sasa na vijavyo,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mwanzilishi na Mhariri Mkuu wa Jarida la Chakula, Kilimo, Lishe na Maendeleo la Afrika, Prof. Ruth Oniang’o alisema anaamini ndani ya muda mfupi ujao, Tanzania itakuwa mfano kwa mataifa mengine kutokana na hatua inazopiga kwenye kilimo.
Prof. Oniang’o alikuwa akichangia mada ambapo alisifu jitihada za serikali zilizofanyika ikiwemo uwekezaji mkubwa katika miundombinu, kubuni miradi ya Jenga Kesho Bora (BBT) na kuwatumia maafisa ugani.
Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, Balozi wa Tanzania Washington, Dkt. Elsie Kanza na watendaji wengine wa Serikali.




