Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Mwigulu:Lipeni fidia kabla ya kutwaa maeneo ya wananchi


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameziagiza Wizara za Kisekta, Taasisi na Mamlaka za Serika za Mitaa zihakikishe zinalipa fidia kwa wananchi wanaopisha maeneo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali kabla ya kutwaliwa kwa maeneo yao kwa kuzingatia taratibu zilizopo.

“Baadhi ya maeneo unakuta mwananchi mnyonge, mwananchi wa kawaida ametoa eneo limejenga kituo cha afya, limejenga shule na anachodai ni kidogo tu miaka yote ameendelea kudai hajalipwa. Mheshimiwa Rais alishaelekeza pamoja ya kuwa tunataka miradi ya maendeleo, tunataka uwekezaji tusipore maeneo ya wananchi kwa vigezo hivyo bila ya kuwalipa fidia.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya Serikali watimize wajibu wao kwa mujibu wa mikataba waliyoingia ikiwa ni pamoja na kuwalipa watoa huduma walioshiriki kwenye utekelezaji wa mradi husika.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Aprili 1, 2026) wakati akiwasilisha hotuba yake kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo kufuatia malalamiko mbalimbali ya wananchi wanaodai kuchukuliwa maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali bila ya kulipwa fidia.

Kuhusu wakandarasi amesisitiza ubora wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa uwiane na thamani ya fedha iliyotolewa, pia Waziri Mkuu amewataka maafisa masuuli wahakikishe wazabuni na watoa huduma wanalipwa kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano na huduma iliyotolewa.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza mamlaka zinazohusika na masuala ya wakandarasi kuwawajibisha baadhi ya wakandarasi kutoka nje ya nchi ambao wanashindwa kuwalipa kwa wakati wakandarasi wa ndani.

“…fedha zinazoelekezwa na Serikali kwenye miradi hiyo zitumike kama ilivyokusudiwa. Vilevile, wakandarasi wa ndani wawe wazalendo kwa kutumia ipasavyo fursa inayotolewa ya ushiriki wa kampuni zilizosajiliwa ndani kutekeleza miradi mikubwa.”

Vilevile, Waziri Mkuu amezielekeza taasisi zote za umma kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali ikiwemo mipango, programu na miradi ili kuongeza tija ya utendaji kazi na kuboresha huduma kwa wananchi.

Aidha, Waziri Mkuu amezitaka Wizara, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi, Wakala na Idara zinazojitegemea kuanza kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi trilioni 12.50 kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 8.73 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 3.76 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Fedha hizo ni kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2026/2027.

Vilevile, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi 225,021,780,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 207,992,798,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 17,028,982,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.