Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Prof. Kabudi Atembelea Miradi ya VVU na UKIMWI Mkoa wa Morogoro Inayoratibiwa na TACAIDS.


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amefanya ziara katika Mkoa wa Morogoro ili kuangalia Miradi inayotekelezwa na TACAIDS chini ya Uratibu wa  Ofisi ya Waziri Mkuu-SBUU kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro. 
Katika ziara hiyo, Waziri Prof. Kabudi aliweza kutembelea kituo cha Afya Kingolwira, kiliboreshwa kupitia miradi ya VVU na UKIMWI iliyoratibiwa na TACAIDS kwa kuongezewa jengo la maabara na jengo la kuchomea taka. Kituo hicho ni kati ya vituo 32 nchini ambavyo vilinufaika na miradi ya VVU na UKIMWI iliyoratibiwa na TACAIDS.

Aidha, katika hatua nyingine, Waziri Prof. Kabudi alitembelea mashine zinazotoa huduma za kinga na upimaji wa VVU kwenye maeneo ya vyuo vikuu vya Mzumbe na cha Kilimo SUA vilivyopo mkoani humo. Mashine hizo zinazojulikana kama Digital Vending Machine zimekua zikitoa huduma ya kondomu za kiume na za kike pamoja na Vitepe vya JIPIME. Waziri Prof. Kabudi amewaasa vijana kuendelea kutumia huduma za VVU na UKIMWI kwani serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya juhudi kubwa za kuweka mashine hizo katika vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na chuo Mipango, CBE, UDOM pamoja na Hombolo jijini Dodoma.