Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Dhana ya Afya Moja

Utangulizi

Afya Moja ni dhana ya kimataifa iliyoridhiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Programu ya Kimataifa ya Mazingira (UNEP) kupitia “Global Health Security Agenda” (GHSA) na wadau wengine wa Afya duniani kote. Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) yamekuwa yakishirikiana duniani kote na kutoa wito kwa wataalamu wa sekta za Afya ya Binadamu, Wanyama na Mazingira kuongeza na kuimarisha ushirikiano na mawasiliano ili kuboresha ufanisi katika kukabiliana na tishio la magonjwa ya kuambukiza yanayoenea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na yanayovuka mipaka; tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa na changamoto zingine zinazokabili afya ya jamii zinazohitaji nguvu ya pamoja..

Lengo la Dhana ya Afya Moja

Lengo la dhana hii ni kupanua na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta/taaluma mbalimbali katika hatua zote za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali. Ushirikiano huu pamoja na wadau wengine ikiwemo jamii, kimsingi unaongozwa na sekta/wizara za msingi (lead Ministries) ambazo ni Afya ya Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori), Mazingira na Kilimo katika ngazi zote.

Muundo wa usimamizi

Kwa mujibu wa Muundo wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dawati la Uratibu wa Afya Moja lipo chini ya Idara ya Menejimenti ya Maafa ambayo utekelezaji wa majukumu yake unaongozwa na Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 inayoweka umuhimu katika usalama wa maisha ya watu na mali zao kwa kupunguza athari za kiuchumi na kijamii. Aidha, ili kuipa nguvu Sera ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004, Serikali ilitunga Sheria ya Usimamizi ya Maafa Namba 7 ya Mwaka 2015 inayosimamia utekelezaji wa shughuli za idara.

Majukumu

1.Kuratibu na kusimamia shughuli za Afya Moja kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji zinazojumuisha:

  • Kuzuia, kufuatilia, kujiandaa, kukabiliana na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza yanayoenea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu (Zoonotic Diseases) na yasiyo ya kuambukiza (NCDs);
  • Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa;
  • Usalama wa Chakula;
  • Ulinzi na Usalama wa Vimelea vya Magonjwa; na changamoto zingine zinazoathiri afya ya binadamu, mifugo, wanyama pori na mazingira zinazohitaji ushirikiano baina ya sekta na taaluma mbalimbali.

2.Kuratibu vikao vya Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa Masuala ya Afya Moja;

3.Kuandaa Mipango, Mikakati, Miongozo na Machapisho kwa ajili ya utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja nchini; na

4.Kuandaa mikakati ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uetekezaji wa shughuli za afya moja.

Aidha, Dawati la Uratibu wa Afya Moja linatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Wizara, Idara na Taasisi za serikali na sizizo za kiserikali, Mashirika ya Kimataifa na wadau wengine wa maendeleo