Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mhagama afurahishwa na wanufaika Mafunzo ya Uanagenzi VETA Pwani.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameridhishwa na maendeleo ya wanufaika wa mafunzo ya uanagenzi yanayotolewa kwa lengo la kukuza ujuzi katika fani mbalimbali kwa vijana mkoa wa Pwani.

Ameyasema hayo alipotembelea na kukagua shughuli za utekelezaji wa program hiyo katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani ambapo aliridhishwa na hatua na mafanikio kwa wanafunzi waliojiunga katika fani mbalimbali ikiwemo, Ufundi wa kushona, useremala,kutengeneza majokofu na viyoyozi, ufundi umeme wa majumbani na umeme wa magari mapema mwanzoni mwa wiki.

“Nimefurahishwa na kundi la vijana kujitokeza kuongeza ujuzi bila kujali viwango vya elimu zao, kwani katika awamu hii, wapo walioshindwa kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na wahitimu wa elimu ya juu wanaoendelea na mafunzo ya ufundi stadi hapa VETA”, aieleza Waziri Mhagama.

Aidha alizipongeza jitihada za uongozi wa Chuo kwa kushirikiana na Ofisi yake kuweza kuendesha mafunzo hayo kwa kuamini yatasaidia kuendeleza jitihada za kutatua changamoto za ajira nchini.

“Nimekuja kutizama maendeleo ya mafunzo haya na kuona changamoto zinazowakabili ili kuzitatua kwa namna bora na kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki ya kujifunza kulingana na umuhimu wa mafunzo na kuyafikia malengo tuliyojiwekea,”alisema

Pamoja na hayo, Waziri aliutaka uongozi wa mkoa kuona umuhimu wa kuendeleza jitihada hizo ikiwemo ya kuhakikisha wale wote waliostahili kuwepo katika mafunzo hayo wanahudhuria bila kukosa na kujitahidi kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wao.

Akiwasilisha taarifa ya chuo hicho pamoja na utekelezaji wa programu hiyo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Bi.Clara Kibodya alieleza mafanikio ya uwepo wa mafunzo ambapo, vijana wameweza kupata ujuzi, walimu kupata fursa ya kuzitumia fani zao, ongezeko kubwa la vijana wa kike hasa katika fani zilizoaminika na jamii kuwa za kiume pamoja na mafunzo kusaidia kupunguza wimbi la vijina wasio na ajira.

 “Kupitia fedha zinazotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu wanafunzi wamenufaika kusoma kwa uhuru na kuchochea mwitikio wa kujiunga ambapo awamu hii kundi la vijana wa kike limekuwa kubwa hasa katika fani ya ufundi wa magari na umeme wa majumbani,”alisisitiza Clara

Akitoa neno la shukran kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Ezrom Makau anayesomea ufundi wa magari aliishukuru Serikali kuwakumbuka vijana bila kujali tofauti zao.

“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa programu hii kwani ni fursa nzuri ya kupata ujuzi katika fani mbalimbali zitakazotusaidia kuongeza ujuzi utaosaidia kutatua changamoto za ajira na kuchangia kukuza uchumi wetu,”alisema Makau

AWALI

Chuo Ufundi Stadi cha VETA Pwani kilifunguliwa tarehe 21 Machi, 2012 kinachotoa mafunzo ya ufundi stadi katika maeneo mbalimbali ikiwemo; fani ya umeme wa majumbani, wa magari, ufundi wa majokofu na viyoyozi, ufundi wa vifaa vinavyotumia umeme mdogo, ushonaji na ubunifu wa mitindo, maabara. Kwa awamu hii chuo kilipangiwa jumla ya vijana 120 kwa awamu ya kwanza na 72 wa akiba katika fani sita. Programu ya Uanagenzi inayoratibiwa Idara ya Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu imelenga maeneo manne ikiwemo; Mafunzo ya uanagenzi, kurasimisha ujuzi usio rasmi, mafunzo ya kujenga uzoefu, kuongeza ujuzi kwenye teknolojia mpya na mabadiliko mapya ya maeneo ya kazi.

=MWISHO=