Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Kamilisheni Miradi kwa wakati-Dkt. Mwigulu


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewaagiza wakandarasi na wasimamizi wa miradi ya maendeleo nchini kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, ili wananchi waweze kunufaika.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Machi 13, 2026), wakati akiweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Kata ya Shanwe, Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo, hivyo ni muhimu kwa wakandarasi na wasimamizi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuwahudumia wananchi.

“Endeleeni kufanya kazi kwa bidii, ikiwezekana fanyeni kazi mchana na usiku ili mradi huu ukamilike mapema na wananchi hawa wapate maji safi na salama,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Manispaa ya Mpanda, ambapo huduma ya maji inatarajiwa kufikia asilimia 100.

Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 22.8 umefikia asilimia 55 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Julai, 2026.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Mathew Kundo, alisema kwamba mradi huo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha takribani lita milioni 12 za maji kwa siku, jambo litakaloimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.

Amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Miji 28 nchini, ikiwemo wa Mpanda, ni ishara ya mapinduzi makubwa katika sekta ya maji. “Mradi huu wa Miji 28 hapa Mpanda unategemea kuhudumia takribani wananchi milioni 6 na utaongeza asilimia 8 katika gridi ya Taifa ya Maji.”

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kufikisha huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Mpanda kwa asilimia 100. “Kwa hapa Mpanda zaidi ya Watanzania 200 wamepata ajira kutokana na kutekelezwa kwa mradi huu.”