Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu achukizwa ukosefu wa Dawa Tanganyika


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu  Nchemba  amemuagiza Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Sipha Mwanjala, kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mtiririko wa fedha za ununuzi wa dawa pamoja na upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani humo.

Ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Machi 13, 2026, alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Masemba Nane Nane, eneo la Majalila Wilayani Tanganyika akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo Mkoani Katavi.

Waziri Mkuu amesema taarifa zilizopo zinaonesha kuwa upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya unafikia zaidi ya asilimia 90, lakini wagonjwa wanapofika hospitalini wanakosa dawa na kuelekezwa kwenda kuzinunua katika maduka binafsi ya dawa nje ya hospitali 

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini mtiririko wa fedha za dawa pamoja na mfumo wa upatikanaji wa dawa katika vituo hivyo.

Hii michezo haikubaliki. Zinakujaje fedha za dawa na tunaambiwa utoshelevu ni zaidi ya asilimia 90, mgonjwa anakosa dawa? Kamanda wa TAKUKURU fanya uchunguzi wa mtiririko wa dawa na fedha zinakokwenda.

Pia, Waziri Mkuu ameagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi katika miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Tanganyika ili kubaini namna fedha zilizotolewa na Serikali zinavyotumika na kuhakikisha uwajibikaji kwa wahusika.

Katika maelekezo yake, Dkt. Mwigulu amehoji uwezekano wa maduka binafsi kuwa na dawa wakati hospitali za Serikali zinakosa licha ya kutolewa fedha za ununuzi wa dawa.

Inakuwaje duka la mtu binafsi anapata dawa huku Serikali inakosa? Huo ni mchezo na kamanda wa TAKUKURU fanya uchunguzi wa upatikanaji wa dawa na mtiririko wa fedha za dawa. Taarifa nzuri zinatolewa lakini kila mgonjwa anaelekezwa nje kwenda kununua dawa."

Amesema katika Wilaya ya Tanganyika, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.062 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo haikubaliki kuona wananchi wanakosa dawa wanapokwenda kupata matibabu.

Awali, Dkt. Mwigulu ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya Kagwira – Karema (kilometa 112) katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.
 
Mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 219.09, ukiwa na lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyosomwa na Kaimu Meneja wa Udhibiti wa Miradi TANROADS, Mhandisi Malima Musema Mongo, ujenzi wa barabara hiyo umegawanyika katika vipande viwili ambavyo ni Kagwira – Kasekese (kilometa 54.144) na Kasekese – Ikola – Karema (kilometa 56.911).
 
Alisema ujenzi wa kipande cha Kagwira – Kasekese unagharimu takribani shilingi bilioni 106.95 na umefikia asilimia 8.2 ya utekelezaji, huku kipande cha Kasekese – Ikola – Karema kikigharimu takribani shilingi bilioni 112.14 na kufikia asilimia 33.4 ya utekelezaji.