Habari
Dkt. Yonazi aongoza mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM)
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa inayosimamia na kuratibu fedha za Global Fund inayojulikana kama Tanzania National Coordinating Mechanism – (TNCM) ameongoza Kikao cha (TNCM) kilichofanyika katika Ukumbi wa Serengeti, Jengo la FCC, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, mambo mbalimbali yamejadiliwa ikiwemo maandalizi ya awali ya kuandaa andiko la maombi ya ufadhili wa awamu ya nane ya Mfuko wa Dunia (Global Fund Grant Cycle 8 - GC8). Aidha, Dkt. Yonazi amesisitiza umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti na yenye tija ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na rasilimali hizo katika mapambano dhidi ya magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu, na Malaria, pamoja na kuimarisha mifumo ya afya kwa ujumla.
Akifunga mkutano huo, Dkt. Yonazi amewahimiza wajumbe na wadau wote kuendeleza ushirikiano na uwazi (Transparency) katika hatua za maandalizi ya GC8, huku akibainisha kuwa ufanisi wa (TNCM) unategemea sauti ya pamoja ya wadau wote wanaowakilishwa.
Mkutano huo uliowahusisha wadau kutoka Serikalini, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, na Washirika wa Maendeleo, umelenga kujadili masuala mtambuka ya uendeshaji wa taasisi hiyo pamoja na kuweka misingi imara ya upatikanaji wa rasilimali katika sekta ya afya nchini.
Mbali na hayo, katika mkutano huo, wajumbe walimchagua Bw. Godlisten Moshi kuwa Makamu Mwenyekiti mpya wa (TNCM) ili kukamilisha safu ya uongozi na kuongeza ufanisi katika utendaji wa chombo hicho.




