Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Watumishi sita Missenyi matatani kwa ubadhirifu


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza watumishi sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi wafuatiliwe ili warejeshe fedha za umma na kisha wachukuliwe hatua za kinidhamu.

“Uongozi wa Mkoa uendelee kuwafuatilia na kuisimamia Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi ili warudishe fedha za makusanyo za Julai na Agosti, 2023.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo jioni (Jumamosi, Septemba 23, 2023) wakati akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa katika tarafa ya Bunazi, wilayani Missenyi, mkoani Kagera. 

Amewataja watumishi hao kuwa ni Chrispin Mbuga, Andrephnus Kalisa, Nashrath Buyungilo, Lusiana Irunde, Issack Sadick na Willington Mutabilwa ambao ni watoza ushuru wa Halmashauri na kwa pamoja wanadaiwa sh. milioni 37.3. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa Halmashauri kuikosesha Serikali mapato kwa makusudi. 

“Hapa Bunazi kuna mnada wa kimataifa lakini watumishi wa umma walikuwa wanakusanya sh. 30,000 kwa siku na siku ya pili ikapanda hadi sh. 100,000 lakini wakarudi tena kwenye sh. 30,000. Huu ni wizi wa mchana kweupe. Hauvumiliki.

“Rais wetu kasema tusivumilie wezi wanaokuja Halmashauri kwa sababu fedha nyingi inaletwa huko isije kuwa inapotea na mapato yanayokusanywa yasipotee.”

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Wilson Sakulo kwa kuamua kutembelea gulio hilo na kufanya majaribio ya kukusanya mapato ambapo yalipanda kutoka sh. 30,000 hadi sh. 2,050,000 kwa siku. 

“Mkuu wa Mkoa hatua ulizochukua za kuwapeleka mahakamani watumishi watatu wa kwanza ni sahihi, hawa watu wachukuliwe hatua kali sana, tukiwaacha tutafika tumechoka.”

Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu.