Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

“Wananchi tembeleeni banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, tupo tayari kuwahudumia” Dkt. Yonazi


Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imejipanga kuhakikisha inaendelea kuwafikia wananchi wanaopata huduma katika banda jumuishi la ofisi hiyo wakati wa maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba kwa kuhakikisha wanapewa elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu ofisi hiyo pamoja na taasisi zilizochini yake.

Ameyasema hayo tarehe 04 Julai, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ikiwemo la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Fedha na taasisi zake, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Kampuni ya simu ya halotel pamoja na Shirika la posta.

Aidha, Dkt. Yonazi ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kutembelea banda hilo na kupongeza namna watumishi wa ofisi hiyo wanavyoendelea huwahudumia wananchi na wadau wanaofika huku akiwasii watumishi hao kuendelea kuzingatia weledi zaidi katika utoaji huduma na elimu kwa umma.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya uratibu pamoja na huduma zinazotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu hivyo wananchi na wadau mbalimbali wayatumie maonesho hayo kama fursa yakujifunza kuongeza uelewa” alisema Dkt. Yonazi

Maonesho hayo ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania: Mahali Sahihi Pa Biashara na Uwekezaji,”.

 

=MWISHO=