Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Tanzania yashika nafasi ya nne Afrika kwenye usalama wa anga


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania imefanikiwa kushika nafasi ya nne barani Afrika kwenye masuala ya usalama wa anga kwa kupata alama 86.7 ikitanguliwa na Nigeria, Kenya na Ivory Coast katika ukaguzi uliofanyika Mei, 2023.

“Kwenye ukaguzi mwingine wa uwezo wa nchi kiusalama uliofanywa na Shirika la ICAO, viwanja vya ndege vya KIA, Zanzibar na JNIA Dar es Salaam vilikaguliwa na kupata alama 86.7. Hatua hiyo, imewezesha nchi yetu kushika nafasi ya nne Barani Afrika ikitanguliwa  na nchi za Nigeria, Kenya na Ivory Coast. Huu ni ushahidi tosha kwamba uwezo wa nchi yetu katika kudhibiti usalama wa anga unaendelea kuimarika,” amesema. 

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 30, 2023) wakati akifungua maadhimisho ya miaka 20 ya TCAA kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 

Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi huo, amesema Tanzania imeweza kuongeza uwezo wa udhibiti wa sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini kwa viwango vya kimataifa. 

“Kupitia kaguzi za Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini, imeongeza uwezo kutoka asilimia 37.8 mwaka 2013 hadi asilimia 69.04 mwaka 2019. Kutokana na ufaulu huo, ICAO imetoa ufadhili wa dola za Marekani milioni moja ambazo zilitumika kwenye mradi wa kuendelea kuboresha uwezo wa usimamizi wa anga letu.”

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni ongezeko la mchango wa sekta ya uchukuzi katika Pato la Taifa huku akibainisha kuwa katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo, sekta hiyo ilichangia asilimia 8.2 ya pato la Taifa kwa mwaka 2022.

“Sekta hii pia imeendelea kuwezesha ukuaji wa sekta nyingine katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo sekta za utalii, biashara n.k,” amesema na kuongeza kuwa jitihada mbalimbali za Serikali katika kuboresha sekta ya usafiri wa anga zimesaidia kuongeza idadi ya abiria na mizigo inayosafirishwa nchini. 

Akitoa mfano wa ongezeko hilo katika kipindi cha miaka 10, Waziri Mkuu amesema: “Jitihada za Serikali zimechangia ongezeka la abiria na mizigo inayosafirishwa ndani na nje ya nchi ambapo idadi ya abiria imeongezeka kutoka  1,662,452 mwaka 2003 hadi abiria 4,614,380 mwaka 2023. Aidha, mizigo imeongezeka kutoka tani 33,255 mwaka 2003 hadi tani 55,806.20 mwaka 2023.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi na viongozi mbalimbali walioshiriki maadhimisho hayo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema anaamini kuwa ukifanyika ukaguzi mwingine, Tanzania itafikisha alama zaidi ya 90.

Alisema Serikali inaendelea na ufungaji wa mitambo ya kuongoza ndege kwenye viwanja vya ndege vilivyoko Pemba, KIA, Mwanza, Songwe na Arusha. “Ninaamini sekta hii itapiga hatua kwa kasi zaidi katika kipindi kifupi kijacho,” alisema. 

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Hamza Johari alisema taasisi hiyo ilianzishwa rasmi Novemba Mosi, 2003 na inatoa huduma za uongozaji ndege katika viwanja 15 hapa nchini.

Amevitaja viwanja hivyo kuwa ni Arusha, Geita, Dodoma, Kigoma, Mtwara, Mwanza, Zanzibar, Pemba, Dar es Salaam, Songea, Songwe, Iringa, Tanga, Tabora na Bukoba ambako hivi karibuni wamefunga mitambo ya kuongoza marubani wakati wa hali mbaya ya hewa.