Habari
Prof. Kabudi Akabidhi Bajaji kwa Mkazi wa Msalato
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, amemkabidhi bajaji Bw. John Miina Mpumpa, mkazi wa Msalato, Mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwawezesha watu wenye ulemavu kujitegemea kiuchumi.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo, , katika Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ngome, jijini Dodoma. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Prof. Kabudi alisema Serikali itaendelea kuweka mbele ustawi wa watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanapata fursa na mazingira jumuishi yanayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Alieleza kuwa uwezeshaji huo unaakisi dhamira ya Serikali ya kuboresha maisha ya wananchi wenye mahitaji maalum kupitia hatua mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Bajaji hiyo ilitolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo S. Nyansaho, kufuatia ombi la msaada lililowasilishwa Serikalini na Bw. Mpumpa.
Prof. Kabudi pia alimpongeza Bw. Mpumpa kwa uzalendo wake na mchango alioutoa kwa taifa wakati wa kipindi chake cha utumishi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuthamini wananchi walioitumikia nchi kwa uadilifu na kujituma.
Kwa upande wake, Bw. Mpumpa aliishukuru Serikali kwa kuendelea kumjali na kumpatia msaada huo, akisema utamwezesha kujipatia kipato na kuboresha maisha yake licha ya changamoto za kiafya anazokabiliana nazo.




