Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu: Wakandarasi warudi site


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameelekeza wakandarasi waliokuwa wamesimamisha kazi katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara mkoani Mara kurejea maeneo ya kazi mara moja, huku Serikali ikiendelea kuwalipa ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Serengeti, Tarime Mjini, mkoani Mara, leo Alhamisi (Julai 2, 2026), Waziri Mkuu alisema Serikali imeweka utaratibu mpya wa kuhakikisha fedha za Mfuko wa Barabara zinapelekwa moja kwa moja kwenye mifuko husika ili kuondoa changamoto ya kuchelewa kwa fedha za utekelezaji wa miradi.

 "Serikali imepitisha uamuzi kwamba sasa fedha za Mfuko wa Barabara hazitapitia Mfuko Mkuu. Zitakwenda moja kwa moja kwenye mifuko ili barabara hizi ziweze kujengwa."

Aidha, Waziri Mkuu alisema tayari amemuelekeza Waziri wa Ujenzi kuwaita wakandarasi wote waliosimamisha kazi warejee site na kuendelea na utekelezaji wa miradi ya barabara ikiwemo Tarime–Mogabiri, Tarime–Mugumu, Sanzate–Nata, Nyamongo–Mugumu na Mogabiri–Nyamongo.

"Nimemuelekeza Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi waite wakandarasi ambao walishaondoka site, warudi site na endeleeni kuwalipa fedha waendelee kutekeleza hii miradi."

Alisema kuchelewa kwa baadhi ya miradi hakukutokana na kupuuzwa kwa maeneo husika, bali ni uamuzi wa Serikali wa kuelekeza rasilimali katika kukamilisha miradi ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, ambao sasa umeongeza upatikanaji wa umeme nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali imeweka asilimia tano ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kujenga miundombinu ya biashara na kununua maeneo ya kimkakati kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, vijana na wanawake.

 "Kuanzia sasa sitarajii machinga, mamalishe na vijana wanaofanya shughuli mbalimbali za biashara kupelekwa maeneo yasiyofaa. Kama wanahitaji eneo la kimkakati, litumieni asilimia tano hiyo kulinunua."

Pia alisema Serikali itawasilisha bungeni marekebisho ya sheria ya kutaifisha mifugo kwa lengo la kuondoa adhabu zisizo na uwiano kwa wafugaji na kuendelea kulinda shughuli za uzalishaji.

Aidha, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali imepiga marufuku kukamatwa kwa vitendea kazi vya wananchi kwa madai ya faini, akieleza kuwa hatua hiyo imekuwa ikikwamisha shughuli za uzalishaji na kujiongezea kipato.

"Kama jambo ni la faini, acheni kukamata vitendea kazi vya Watanzania. Waacheni wafanye kazi."

Sambamba na hayo, Waziri Mkuu alitoa wito kwa viongozi wa Serikali na Chama kujikita katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo badala ya kuanza makundi ya uchaguzi mapema, akisema wananchi wanahitaji huduma na maendeleo, si migogoro ya kisiasa.

Akihitimisha, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa, akisisitiza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Uchaguzi na mipango mingine ya maendeleo utafanikiwa endapo nchi itaendelea kuwa na amani, utulivu na usalama.