Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa aagiza uongezaji thamani mazao ya misitu ufanyike nchini


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa uzalishaji mazao ya misitu kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao hayo hapa nchini badala ya kusafirisha malighafi hizo nje ya nchi.

Amesema kuwa Tanzania kwa sasa inayo teknolojia kubwa ya uchakataji wa mazao ya misitu na utengenezaji wa Samani zake hivyo hakuna haja ya wadau wa misitu kusafirisha mazao hayo kwenda nje kwa ajili ya uchakataji.

"Lazima tuweke ukomo wa uvunaji na uchakataji tunataka kila kitu wamalize hapa hapa kama wanavyofanya TANWAT, wanaanza mwanzo mpaka mwisho wakiwa hapa hapa Tanzania, hapa hapa njombe kwa hivyo na viwanda vingine vibainishwe ambavyo havijakamirisha, tulishawapa muda inatosha"

Ameyasema hayo leo, (Ijumaa 21, Machi, 2025) katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika Mkoani Njombe.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kuendelea kuhamasisha na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika kuanzisha mashamba ya miti na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya misitu. 

Kadhalika ameitaka Wizara hiyo kushirikiana na Mamlaka nyingine kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu kuhusu uhifadhi na biashara ya kaboni ili waweze kuanza kunufaika kupitia biashara hiyo.

"Taasisi za misitu ziweke mipango thabiti ya kukabiliana na uchomaji moto ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia teknolojia katika kutambua na kupambana na moto."

Pia amezitaka, Wizara na Taasisi hizo kuhakikisha zinaboresha ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa sekta ya misitu na jamii inayozunguka maeneo ya misiti ili kuhakikisha mipango na mikakati ya uhifadhi inatekelezwa kwa ufanisi. 

"Wataalamu wa misitu wanapaswa kushirikiana na jamii katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi, ikiwemo kuanzisha mashamba ya misitu, na programu za upandaji miti."

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea kiwanda cha uchakataji mazao ya misitu cha TANWAT (Tanganyika Wattle Company Limited) kilichopo Njombe mjini ambapo alishuhudia shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda hicho.

Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho Waziri Mkuu amewasihi wafanyakazi wazawa kufanya kazi kwa weledi ili kufanikisha malengo ya muwekezaji ili aongeze fursa za ajira zaidi kwa watanzania wengine.

"fanyeni kazi kwa uaminifu, fanyeni kazi kwa uadilifu, na kwa weledi".

Kwa Upande wake waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa ili lengo la kuongeza hamasa na tija katika masuala ya utunzaji misitu, wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau iliona ni vyema maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti kitaifa yakafanyika kwa pamoja. 

Aidha amesema tangu kuanzishwa kwa  maadhimisho hayo yamekuwa ni fursa katika kuchochea juhudi za uhifadhi na upandaji miti kwa jamii na umma mzima wa Watanzania. 

"Tangu 2020 hadi sasa, Wakala umefanikiwa kupanda jumla ya miti zaidi ya milioni 146 ya miti jamii mbalimbali ikiwemo mikoko 1,184,091 imezalishwa na kuoteshwa katika maeneo mbalimbali nchini."

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amesema Mkoa huo unaendelea kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi katika kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kuanzisha mifumo ya kilimo cha kisasa pamoja na uzalishaji wa mbegu za kisasa za viazi mviringo.

Mwaka 2012, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha tarehe 21 Machi ya kila mwaka kuwa siku ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani  na kuwataka nchi mwanachama kuadhimisha siku hii kwa kuzingatia mazingira yake.

Aidha, Siku ya Upandaji Miti Kitaifa iliidhinishwa kupitia Waraka wa Waziri Mkuu Na. 1 wa mwaka 2009 ukielekeza kuwa tarehe Mosi Aprili ya kila mwaka iwe Siku ya Upandaji Miti Kitaifa kwa lengo la kuhimiza, kuelimisha na kuhamasisha Umma wa watanzania kuhifadhi misitu ya aina zote ili kupata faida za bidhaa na huduma. 

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Ongeza thamani ya mazao ya Misitu kwa uendelevu wa rasilimali kwa kizazi hiki na kijacho’’ na Kauli mbiu ya kidunia ni “Misitu na Chakula’’ .