Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Simbachawene, ahimiza mafunzo ya itifaki kuwa endelevu


Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema ipo haja, mafunzo ya itifaki na uratibu wa maadhimisho kufanyika kila mwaka.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene wakati akifunga mafunzo kwa watendaji wa serikali yaliyohusu itifaki ya viongozi wa kitaifa iliyowakutanisha Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa yaliyofanyika Mkoani Singida.

“Mafunzo haya yanapaswa kuongezwa mada na kuongeza namba ya washiriki ili kujenga uelewa wa pamoja”

Ambao utasaidia kupata ufahamu na ujuzi muhimu wa namna ya uandaaji wa Maadhimisho yanayohusu Idara na Taasisi za Serikali kwa Viongozi Wakuu wa Kitaifa na kuzijua kanuni za kiitifaki ambazo mtazitumia katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali kwenye taasisi zenu.

Awali Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bwn. Kaspar Mmuya amesema mafunzo yamelenga kuwa na utaratibu ambao umekubaliwa, ambao unaleta matokeo chanya na watu wote kuheshimu.

“Watendaji waliopokea mafunzo sasa watasaidia katika maeneo yao; kitengo cha maadhimisho Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa sababu ndio Ofisi inayosimamia itifaki za viongozi”.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel  aliyekuwa mtoa maada wa huduma bora kwa mteja; ameshukuru serikali kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamesaidia kuwajenga watendaji kwenda kwa muelekeo unaolengwa na nchi.

“Huu ni uwekezaji  wa kifikira unaofaa, watendaji wakitoa huduma bora kwa wananchi na kwa viongozi, mashauri yatapungua kwa sababu ya huduma kuwa nzuri.”