Habari
WazirI Mkuu: Matokeo ya Sensa yawafikie watendaji wote wa mikoa na halmashauri
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema matokeo ya sensa yanapaswa yawafikie watendaji na walengwa wote katika ngazi ya mkoa na Halmashauri na yawe msingi wa rejea katika kufanya maamuzi yote ya kibajeti, kupanga miradi ya maendeleo na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kisekta.
Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Julai 2, 2024) wakati akizungumza na viongozi, wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria ufunguzi wa Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa Viongozi na Watendaji wa Halmashari za Wilaya za Liwale, Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi uliofanyika kwenye viwanja vya Maonesho, Kilimahewa mjini Ruangwa.
Amesema usambazaji na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa viwe ni ajenda ya kudumu katika vikao vyote vya kikanuni katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri. “Watendaji wote myabebe haya matokeo mkayatumie, muwe viongozi wa kuhakikisha yanatumika.”
Amewataka viongozi na watendaji wakae pamoja na kutafakari namna bora ambayo matokeo ya sensa yanaweza kutumika kubadili hali za maisha ya wananchi pamoja na kuhimiza uwekezaji. “Matokeo haya yanapaswa yatumike na yasaidie kubadilisha maisha ya wananchi huku mkijua kwamba fedha nyingi zimetumika kuifanya kazi hiyo,” amesema.
Akitolea mfano Mkoa wa Lindi, Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa amesema: “Mkoa wa Lindi una fursa nyingi za kuvutia uwekezaji hivyo ni wakati sasa wa kutumia matokeo haya ya sensa kuitangaza Lindi na kuibadili kupitia uwekezaji.”
Amewataka viongozi hao waifanye kazi ya kuhuisha anwani za makazi na kuweka mikakati ya kutunza miundombinu yake kuwa ni endelevu kwa ajili ya kurahisisha ufikiwaji wa wananchi, kurahisisha biashara mtandao, uwekezaji na uwajibikaji. “Kila Halmashauri nchini, ifanye uhakiki wa vibao vilivyowekwa, waelimisheni wananchi umuhimu wake na pia wasiving’oe kwa sababu vinasaidia kuelekeza hata akija mgeni kwa mara ya kwanza hahitaji kuelekezwa na mtu au kuulizia kwa mtu anakokwenda,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande alisema Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwenye ufanyaji wa sensa ya watu na makazi kwa njia ya kidijitali na akasisitiza kuwa watendaji wa Kata na Tarafa watumie ipasavyo matokeo ya sensa kupanga mipango ya maendeleo na waandae zana na ufuatiliaji na tathmini yanayotokana na matokeo ya sensa kwa sababu yanapimika.
Naye, Kamisaa wa Sensa nchini na Spika Mstaafu, Anna Makinda alisema sensa iliyofanyika mwaka 2022 ilikuwa ya aina yake kwa sababu ilikuwa ya kidijitali na ilifanya mambo matatu kwa wakati mmoja ambayo ni kutambua anuani za makazi, kuhesabu majengo na kuhesabu watu.
Mapema, wasilisho la mafunzo hayo lililotolewa kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa lilionesha kuwa kati ya watu milioni 61.7 waliohesabiwa wakati wa sensa, mkoa wa Lindi una watu 1,194,028.
“Kati ya watu 1,194,028 waliopo Lindi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watu wengi (297,676), ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea (Watu 233,655) Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa (Watu 185,573) na Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ni ya mwisho ikiwa na watu 136,505.”
Taarifa hiyo ilionesha kuwa, kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, kata inayoongoza kwa kuwa na watu wengi ni Nachingwea yenye watu 18,343 ikifuatiwa na kata ya Mbekenyera yenye watu 16,531. Kata ya Nandagala ina watu 7,391 wakati kata yenye watu wachache zaidi ni Makanjiro yenye watu 4,002
Kuhusu idadi ya kaya kwa Halmashauri za Mkoa wa Lindi, matokeo ya sensa yanaonesha kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea inaongoza kwa kuwa na kaya 74,738 ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa yenye kaya 72,152. Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ndiyo yenye kaya chache ndani ya mkoa wa Lindi (kaya 35,897). Halmashauri nyingine ni za Wilaya ya Ruangwa yenye kaya 60,931, Manispaa ya Lindi yenye kaya 52,809 na Wilaya ya Mtama yenye kaya 50,708.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni nyenzo muhimu kwa watunga sera, wachumi, maafisa mipango na wadau mbalimbali katika kutunga sera, kupanga na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Matumizi sahihi ya takwimu za sensa katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, kilimo, viwanda na nyingine kwa kuzingatia jinsi, watoto, wanawake, vijana, wazee, watu wenye ulemavu, na makundi mengine yaliyo hatarini kuachwa nyuma ni sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo inasisitiza mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.