Habari
Waziri Mkuu azindua mradi wa maji wa shilingi bilioni 1.3
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji wa Ngulyati - Nyamswa wilayani Bariadi, mkoani Simiyu wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 na kukabidhi mtambo wa kuchimba visima virefu vijijini ambao ni sehemu ya fedha za miradi ya UVIKO-19.
Akizungumza na wakazi wa Ngulyati mara baada ya kuzindua mradi huo leo (Jumamosi, Machi 25, 2023) Waziri Mkuu amesema mradi uliozinduliwa leo ni mojawapo ya malengo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaondolea wananchi adha ya kukosa maji.
“Tangu akiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alianzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani. Rais wetu ameendelea kutoa fedha nyingi za miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi hawapati shida ya maji.”
Ili kutekeleza agizo hilo, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa chombo cha watoa huduma ngazi ya jamii (GAISANGU) wasimamie maji hayo kwenye vilula (viosk) na kuhakikisha yanatoka saa zote bila mgao kwani tenki limejengwa kilimani ili kuwepo na mtiririko wa kutosha.
Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais ametoa magari yenye mitambo ya kuchimba visima ili yatumike kuchimba visima hivyo kwenye maeneo ya vijijini ambako kuna vyanzo vya maji na kwamba walioko mkoani wasiyazuie magari hayo kufanya kazi vijijini.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema: “Kuna mkoa nilienda nikakuta kuna mvutano baina ya RUWASA mkoani na wilayani. Wilayani wanaomba gari likachimbe visima vijijini, wao wa mkoani wanazuia hadi wapewe malipo. Sitaki kuona huo mvutano hapa Simiyu, kikubwa mhakikishe magari yana mafuta, mambo ya malipo mtamalizana baadaye.”
Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa RUWASA, Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala alisema mradi utatoa huduma kwa wananchi 10,106 wa vijiji vya Ngulyati, Nyamswa na Nyasosi na kwamba mahitaji ya maji katika vijiji hivyo vitatu ni lita 271, 900.
Mradi huo ulioanza kujengwa Mei, 2022 na kukamilika Januari, 2023 umeanza kutoa huduma na una uwezo wa kuzalisha maji lita 15,800 kwa saa sawa na kupampu lita 284,000 kwa saa 18 kwa siku.
Kabla ya kwenda Ngulyati, Waziri Mkuu alizindua tawi la NBC wilayani Bariadi ambalo ni la kwanza katika mkoa wa Simiyu.