Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu awaagiza maafisa masuuli wa Serikali kuzingatia vipaumbele vya bajeti ya 2025/2026


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Masuuli katika ngazi zote za umma kuzingatia vipaumbele vilivyoanishwa kwenye Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 iliyopitishwa na bunge.

 Pia, amewaagiza wakamilishe miradi yote ambayo haijakamilishwa sambamba na kutekeleza ahadi za viongozi katika maeneo yao.

 Amesema hayo leo (Alhamisi, Juni 26, 2025) wakati alipotoa hoja ya kukamilisha shughuli za Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma.

 Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa pongezi kwa Wakuu wa Taasisi, watumishi wote wa umma na sekta binafsi kwa kujituma na kutoa ushirikiano mzuri katika kufanikisha shughuli za Serikali. “Hakika jitihada zenu zimewezesha mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi na kijamii”.

 Pia, Waziri Mkuu, amewapongeza wananchi wote kwa juhudi kubwa katika kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali. “Uchumi wa nchi yetu umeendelea kuwa imara wakati wote. Sina shaka hata kidogo upendo wenu kwa serikali ya awamu ya sita umekuwa msukumo wa kujitoa kwenu, Watanzania wenzangu, nikiri kwamba mmeonesha uzalendo, umoja na mshikamano wa hali ya juu uliowezesha serikali kutimiza majukumu yake.”

 Akizungumza kuhusu Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba, 2025, Mheshimiwa Majaliwa ametoe rai kwa watanzania kuhakikisha wanalinda na kuitunza tunu ya amani na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

 “Kwa upande mwingine, Serikali itahakikisha inatekeleza wajibu wake wa kusimamia Katiba, sheria na taratibu zilizowekwa ili kila mwananchi mwenye sifa ya kuchagua na kuchaguliwa aweze kutimiza haki yake ya kikatiba bila vikwazo vya aina yoyote.”