Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu atoa onyo Halmashauri kutochukua viuadudu


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemuelekeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe ahakikishe halmashauri zote ambazo bado hazijachukua viuadudu kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo mwezi Mei zote ziwe zimeshakusanya dawa hizo ili ifikapo mwezi Juni waweze kutekeleza zoezi hilo.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Aprili 2, 2026 wakati akijibu swali la Rose Tweve, Mbunge wa Viti Maalum katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua tamko ya Serikali kuhusu baadhi ya halmashauri ambazo bado hazijatekeleza agizo la chukua viuadudu na kusababisha adha kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa mbunge huyo Mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya ununuzi wa lita 541,666 za viuadudu  ili ziweze kusambazwa katika halmashauri zote nchini, ambapo hadi sasa kuna baadhi hazijachukua dawa hizo huku wananchi wakiendelea kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa malaria.

“…Cha kusikitisha Mheshimiwa Waziri Mkuu kuna baadhi ya halmashauri hazijatekeleza agizo hilo na kusababisha adha kwa Watanzania kwani tatizo la maralia bado linaendelea kupoteza maisha ya Watanzania kwa sababisha vifo hususani kwa wanawake na watoto. Je nini tamko la Serikali kwa halmashauri hizi ambazo bado hazijatekeleza agizo hili?” alihoji.

“Ni kweli kumekuwepo agizo hilo la Serikali katika jitihada za kupambana na maralia kuhakikisha kwamba kunakuwepo na dawa hizo ambazo Serikali imezinunua kwa lengo la kupelekwa kwenye halmashauri zote nchini ili ziweze kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.”

Amesema suala hilo lilishajadiliwa ndani ya Serikali na kwamba ilihitajika yafanyike mafunzo katika ngazi za halmashauri kuhusu utekelezaji wa jambo hilo, kulikuwepo na angalizo la ratiba kwamba jambo hilo liweze kutekelezwa kuanzia mwezi Juni na kuendelea kwa kuwa ni kipindi ambacho maeneo mengi ya nchi yanakuwa hayana mvua.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya jitihada kubwa za kuweza kuhakikisha kwamba mikoa ambayo haijaunganishwa kwa barabara za lami inaunganishwa ili kuweza kuhakikisha mawasiliano pamoja na biashara zinafanyika.

Waziri Mkuu amesema hadi sasa kuna mikoa michache ambayo bado kazi hiyo haijakamilika.  “Natambua kutoka Katavi kwenda Rukwa kulikuwa bado kuna eneo ambalo bado halijaunganishwa kwa lami lakini mkandarasi yuko site kwa ajili ya kuunganisha mkoa wa Rukwa na Katavi, Katavi kwenda Kigoma kulikuwa na sehemu bado haijaunganiishwa kwa lami fedha zipo zoezi hilo litakamilika.”

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mussa Mbuga aliyetaka kujua ni upi mpango wa Serikali katika kuhakikisha barabara zote zinazounganisha mikoa nchini zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi.