Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu ateta na Fumio Kishida, Aishukuru Serikali ya Japan


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemshukuru Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida kwa misaada ambayo nchi yake inaipatia Tanzania ili kuleta unafuu kwenye maisha ya Watanzania.

“Tanzania tunaishukuru sana Serikali ya Japan kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwakwamua wananchi wake kiuchumi na kuwezesha ujenzi wa miundombinu hadi vijijini,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Agosti 27, 2022) wakati akizungumza naye kwa njia ya mitandao kwenye ukumbi wa Palais des Congres, jijini Tunis, Tunisia. Mheshimiwa Kishida ameshindwa kuhudhuria mkutano kwa sababu ya maambukizi ya UVIKO 19.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye anamwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD8) ulioanza leo, alimweleza Waziri Mkuu huyo kwamba Tanzania bado inaomboleza na wananchi wa Japan kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Shinzo Abe na akatumia fursa hiyo kuwapa pole.

Akigusia miradi ambayo Serikali ya nchi hiyo imeisaidia Tanzania, Waziri Mkuu amesema: “Iko miradi mingi ambayo imetekelezwa na Japan kupitia taasisi ya JICA, wako wawekezaji wanafanya biashara nasi na pia yako makampuni ambayo yamejitoa kusaidia sekta muhimu.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuiomba Japan ikamilishe ahadi yake ya kutekeleza miradi waliyoitoa kwenye mkutano wa TICAD 7 ambayo inahusisha ujenzi wa barabara ya Arusha mpaka Holili mkoani Kilimanjaro, mradi wa maji wa Zanzibar, ujenzi wa bandari ya Kigoma na ujenzi wa bandari ya uvuvi Zanzibar.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan, amemtumia salamu Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote na akataka uhusiano wa nchi hizo mbili uimarishwe kupitia taasisi yao ya JICA.

Mapema, akitoa tamko kwa niaba ya Rais Samia kwenye mkutano huo wa kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika, Waziri Mkuu alisema bara la Afrika linakabiliwa na matatizo ya kiuchumi ambayo kwa kiasi kikubwa chimbuko lake ni UVIKO 19.

“Nimewaeleza Wakuu wa Nchi matatizo yanayozikumba nchi za Afrika Tanzania ikiwemo, nimewakumbusha madhara ya UVIKO 19 na matatizo ya vita ya Ukraine na Urusi ambavyo vimesababisha bei za bidhaa nyingi kupanda. Nimewaambia uko umuhimu wa mataifa makubwa ya G20 kuungana na Japan ambayo ni ya tatu kwa ukubwa kiuchumi ili kuzisaidia nchi za Afrika.”

Amesema iko haja ya kuziwezesha nchi za Afrika kujitegemea ili ziweze kuwasaidia wananchi wake kupata fursa za elimu, kujenga uweza wa shughuli za kilimo, utalii ili waweze kukuza uchumi wao.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Rais Tunisia, Mhe. Kais Saied ambapo Rais wa Senegal, Mhe. Macky Sall alitoa hotuba ya ufunguzi na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Kishida Fumio akahutubia kwa njia ya mitandao kutokea Japan.

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo wa siku unatarajiwa kukubaliana kuhusu namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063).

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika.