Habari
Waziri Mkuu apokea majina 453 ya awali walio tayari kuhama Ngorongoro
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea orodha ya majina ya awali ya kaya 86 zenye watu 453 ambao wamekubali kuondoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari yao huku wengine wakiendelea kujiandikisha.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mazungumzo ambayo Waziri Mkuu aliyafanya na wadau wa uhifadhi kwenye vikao vilivyofanyika Februari 14 na 17, mwaka huu kwenye tarafa za Loliondo na Ngorongoro, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.
Waziri Mkuu amepokea majina hayo leo (Alhamisi, Machi 10, 2022) mara baada ya kumaliza kikao na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai (Laigwanak) kwenye mkutano uliofanyika eneo la Oretei Loongaik – Marya, kwenye Chuo cha Ufundi Arusha, jijini Arusha. Eneo hilo hufanyika Bunge la viongozi hao na hutumika pia kufanyia ibada za kimila.
Akikabidhi orodha hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. John Mongela amesema majina hayo ni ya awali na tayari yalishahakikiwa mara baada ya wakazi hao kujiandikisha. “Tutawasimamia vizuri hadi waende kule wapate hati za mashamba, nyumba na maeneo ya kulisha mifugo yao.”
Akizungumza na Malaigwanak hao zaidi ya 350, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara mkoani humo aliliambia Taifa iko hatari ya kutoweka kwa hifadhi ya Ngorongoro ndani ya muda mfupi na akatoa maagizo viongozi waende kuwasikiliza wananchi juu ya hatua za kuchukua ili tunu hiyo isipotee.
“Ile hatari aliyosema Mheshimiwa Rais ni ipi? Zamani watu waliweza kuishi na wanyama bila tatizo kwa sababu kulikuwa na wakazi 8,000 tu wenye ng’ombe 20 hadi 30. Leo hii kuna wakazi 110,000 na mifugo zaidi ya 813,000 wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo.
“Zamani maboma yalikuwa yamesambaa lakini leo hii nyumba zimejaa, tena za bati na tofali. Idadi ya watu imeongezeka, idadi ya mifugo imeongezeka na makazi yameongezeka. Hakuna huduma za afya au shule wakati ni hitaji muhimu kwa wananchi.”
Aliwaeleza viongozi hao kwamba Serikali imetenga eneo wilayani Handeni ambalo limetumika kujenga nyumba, kupima viwanja na kutenga maeneo ya malisho. “Tumepima viwanja 2,406 ambapo kati ya hivyo, viwanja 2,070 tumeandaa kwa ajili ya makazi na kila kimoja kina ukubwa wa ekari tatu. Tumeanza na nyumba 101 za vyumba vitatu vya kulala kwa wale wanaotaka. Tuna viwanja 336 kwa ajili ya huduma kama shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya. Ujenzi wa mifumo ya maji kazi inaendelea.”
“Umeme wa REA pia utakuwepo. Huku mlipo hakuna umeme. Haya tutayafanya na Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza tuyafanye ili wananchi msipate bugudha,” amesema Waziri Mkuu.
Aliwaeleza viongozi hao wa kimila kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia eneo lao la kufanyia ibada za kimila liendelee kutumika kwa sababu ni jambo jema. “Maeneo yote ya kimila, wananchi waruhusiwe kuendesha mila zao. Mkuu wa Mkoa simamia hili, ilimradi Mkuu wa Chuo apewe taarifa mapema kwamba mnakuja lini kufanya shughuli yenu,” amesema.
Mapema, Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Wamasai Tanzania, Bw. Isack Ole Kisongo alisema kwa nafasi yao viongozi wa kimila wako tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote.
“Kwa kunyanyua rungu zetu tumekula kiapo kwa kukubali kuwa Ngorongoro na hifadhi nyingine nchini zilindwe kwa nguvu zote ili hadhi yake irudi kama zamani.”
Alisema suala la kuhama Ngorongoro halina tofauti na maeneo mengine ambako wananchi waliondoka kwa amani kupisha miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa, bomba la Mafuta la kutoka Tanga hadi Uganda na ukuta wa Mererani.
Naye Laigwanan wa Malaigwanani wa Ngorongoro, Mzee Matengway Ole Tauwo alimweleza Waziri Mkuu kwamba anasubiri kwa hamu tarehe ya kuhamia huko kwa sababu ameenda hadi Handeni na ameona kwa macho yake kwamba mipango ya Serikali ina lengo zuri.
“Nataka uniambie leo tarehe gani Mkuu wa Mkoa ananipeleka huko, niko tayari kwenda. Mke wangu alipoona ile nyumba alitaka kugoma kurudi tena Ngorongoro. Nataka nijue tarehe ya kwenda sababu hapa sina hatimiliki, siwezi kulima lakini kule naweza,” alisema mzee huyo mwenye umri wa miaka 70.
Akisoma risala kwa niaba ya Malaigwanak hao, Katibu Mkuu wa Jamii hiyo, Bw. Amani Lukumay alisema wanayo maeneo ya kimila ambayo yametishiwa kuchukuliwa na akaomba Serikali iingilie kati ili maeneo hayo yakabidhiwe rasmi kwao.
-End-