Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu amkaribisha Dkt. Biteko Ofisini


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Septemba 2, 2023 amemkaribisha Naibu Waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu zilizopo Magogoni jijini Dar es Salaam na amemuahidi kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongezea nguvu Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kumteua Mheshimiwa Dkt. Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu ili waweze kusimamia uratibu wa shughuli za Serikali kwa pamoja.

“…Kwa niaba yenu Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu tunakukaribisha sana hapa katika ofisi yetu na tunakupongeza kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kupewa jukumu kubwa la Naibu Waziri Mkuu kwa lengo la kusimamia shughuli za Serikali. Nakuhakikishia kwamba una timu imara ambayo inatoa ushirikiano wakati wote.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano. Amewaomba watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wafanye kazi kwa bidii ili maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia na watanzania yaweze kufikiwa.

Viongozi wengine walioshiriki mapokezi hayo ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako.

Wengine ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe.Ummy Nderiananga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Anderson Mutatembwa.