Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu akagua uzalishaji wa Maji Ruvu Chini


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Desemba 29, 2025 amekagua hali za uzalishaji na usambazaji wa maji eneo la Ruvu Chini, mkoani Pwani na ameiagiza Wizara ya Maji ihakikishe suala la ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda lipewe kipaumbele ili kukabiliana na upungufu wa maji.

Baada ya kukamilisha ukaguzi huo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi, Serikali ilianza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwani maji ni uhai na hayana mbadala.

“Mipango hii ya ujenzi wa miradi inayolenga kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji ilianza miaka mitatu iliyopita kwa kujenga miradi mikubwa itakayotoa matokeo chanya. Serikali haijalala inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.”

Pia, Waziri Mkuu ameagiza kukamilika kwa haraka usanifu wa mradi wa kutoa maji Mto Rufiji ambao ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025/2030 ambayo inaielekeza Serikali kuanzisha Gridi ya Taifa ya Maji kwa kutumia vyanzo vikubwa vya maji kama Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika.

Gridi hiyo itaenda kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya nyumbani pia mengine kwa ajili ya mifugo na shughuli za umwagiliaji ambapo mradi mkubwa utakuwa wa bomba kutoka Ziwa Victoria hadi mkoani Dodoma likipita mkoani Singida likiwa na njia mbili ya maji ya kunywa na ya kilimo na mifugo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema kuwa kutokana na mabadiliko tabia ya nchi, uzalishaji wa maji katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) ulipungua kutoka mita za ujazo 534,600 zilizokuwa zinazalishwa kwa siku hadi kufikia mita za ujazo 270,000 kwa siku ikiwa ni upungufu wa mita za ujazo 264,600 kwa siku.

Waziri Aweso amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali iliweka jitihada za kufufua visima mbalimbali kwenye eneo la huduma la DAWASA na kuviunganisha na mtandao wa maji wa DAWASA. Pia, Serikali imefanyika kazi kubwa ya kurudisha Mto Ruvu kwenye njia yake ya asili eneo la Kitomondo – DAWASA.

Amesema ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika kipindi cha muda mrefu, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda wenye gharama ya shilingi bilioni 336, utekelezaji wake umefika asilimia 40.

Waziri Aweso ameongeza kuwa miradi mingine inayoendelea kutekelezwa pamoja kutoa maji Mto Rufiji eneo la Mloka kwa lengo la kuhakikisha DAWASA inakua na maji ya kutosha na kuanza utekelezaji wa mradi wa Kimbiji awamu ya pili.