Habari
Waziri Mkuu ahesabiwa Kijijini Namahema
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema amefarijika na jinsi zoezi la sensa ya watu na makazi lilivyoanza mwaka huu na kupokelewa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa kweli nina faraja sana kwamba kati ya sensa zilizofanyika hapa nchini, hii ya mwaka huu Watanzanua wameipokea vizuri na wamehamasika sana,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 23, 2022) mara baada ya kumaliza kuhojiwa na karani wa sensa nyumbani kwake kijiji cha Namahema, kata ya Nandagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Amesema anawashukuru viongozi wakuu wa Kitaifa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa hamasa walizotoa wakati wa zoezi zima la kuhamasisha umma.
“Pia ninawashukuru sana viongozi wa dini kwa kutoa hamasa kupitia nyumba za ibada na kipekee zaidi vyombo vya habari ambavyo vimefanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi.”
Amesema sensa ya mwaka huu ni ya aina yake kwa sababu inajumuisha uratibu wa mfumo wa anuani za makazi ambao haukuwepo kwenye sensa tano zilizotangulia na pia inaenda kwa mifumo ya kidigitali ambapo mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHEMA) inatumika.
“Awamu tano zilizopita huyu karani hapa angekuwa na makaratasi mengi ya madodoso kibao lakini kutokana na mfumo huo ana kifaa kimoja tu ambacho kimebeba maswali yote. Mimi hapa nimejibu maswali 100 ndani ya muda mfupi kwa kutumia kifaa hicho.”
Amewataka wananchi ambao hawajafikiwa wasiwe na hofu kwani sensa hii ina maswali madogomadogo ambayo hayalengi kuleta tafrani bali yenye kulenga kupata taarifa za kuisaidia nchi kupanga mipango ya kuleta maendeleo.