Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mhagama azindua Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikai masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amezindua Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Tarehe 4/10/2021 Mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa uzinduzi waziri alieleza kuwa bodi hiyo imeundwa kisheria ambapo ina majukumu ya kusimamia maslahi ya Wanachama kama kazi mojawapo ya Bodi, kwa mujibu wa Sheria wanachama hao ni pamoja na waajiri na wanufaika ambao ni wafanyakazi.

Kazi nyingine ni kusimamia sekta husika na kushauri katika masuala ya Sera zinazohusu uendelevu wa Mfuko na Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini.

Alieleza jukumu jingine ni kusimamia matumizi ya mifuko katika sekta ili yasiwe makubwa kuzidi lengo kuu la mifuko ambalo ni kulipa mafao ya wanachama wao kwani ikiwa matumizi ya mfuko ni makubwa kuliko mapato mfuko huo hauwezi kufikia malengo yake ya kutoa mafao kwa wanachama.

“Bodi inalo Jukumu lingine la kusimamia mali za mfuko, Bodi ina mamlaka kisheria kushitaki na kushitakiwa, kwa hiyo inalo jukumu kubwa la kuingia mikataba yenye tija kwa ajili ya maslahi ya mfuko,”alisema waziri.

Waziri alitumia nafasi hiyo kumpongeza Bw. Emmanuel Humba kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) huku akimsihi kuendelea kuusimamia Mfuko kwa kushirikiana na Menejimenti ili kufikia matarajio ya Serikali kama ilivyokusudiwa.

“Historia na utendaji wako wa kazi ni kielelezo tosha kuwa wewe ndio chaguo sahihi kwa wakati huu tulionao, kuulea na kuuongoza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kupitia Bodi yako ya Wadhamini. Unastahili,tunajivunia na ninakupongeza sana,” alisema waziri Mhagama.

Aidha alieleza kuwa, Bodi hiyo ni  chombo cha juu cha maamuzi kuhusu Mfuko ambapo utekelezaji wa siku hata siku umekasimiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko ambaye pia ni Katibu wa Bodi.

“Ninayo imani kubwa sana na Bodi hii kwa sababu ninaelewa uwezo, uzoefu na umahiri wenu utasaidia katika kuimarisha zaidi Mfuko wetu wa Fidia kwa Wafanyakazi,”alisisitiza.

Waziri Mhagama aliwataka wajumbe hao kuyaelewa vema majukumu yao kama yalivyoanishwa kisheria katika kifungu cha 13, 14, 15 na 16, na kuendelea kuwasihi kuzingatia sheria na taratibu zinazoongoza chombo hicho ili kuyafikia malengo.

Pia, alitumia nafasi hii, kuipongeza Bodi ya Wadhamaini ya WCF ambayo ilimaliza muda wake tarehe 22 Januari 2018 na kutambua mchngao wako kuifikisha bodi mahali pazuri.

“Katika kipindi hicho, thamani ya Mfuko imekua kufikia shilingi za Kitanzania bilioni 445.49 (kwa mujibu wa hesabu za sasa) ukilinganisha na mwaka 2016/17 ambapo thamani ya mfuko ilikuwa TZS.112.83,”

Aidha, alieleza kuwa suala la ulipaji wa mafao kwa wanufaika wa Mfuko nao umeongeza hadi kufikia shilingi za Kitanzania bilioni 12.43 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kulinganisha na kiasi cha shilingi bilioni  1.55 kilicholipwa katika mwaka ulioishia Juni 2017 na kuendelea lupongeza juhudi hizo.

Akitoa neno la shukran, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Emmanuael Humba alimshukuru waziri kuona umuhimu wa kuzindua bodi hiyo na kumwakikishia kuwa, watekeleza maagizo na maelekezo ya Serikali ili kutimiza majukumu kwa weredi na juhudi kwa kuzingatia kundi wanalolihudumia.

Naye Bw. Tumaini Nyamhoya rais wa TUCTA alipongea na kutumia fursa hiyo kuwaasa wafanyakazi wote nchini kukwepa migogoro sehemu zao za kazi na badala yake kuleta hoja mezani na kutafuta ufumbuzi.

“TUCTA inaunga mkono jitihada hizi na hii ni fursa kwa wafanyakazi kuendelea kutumia mfuko huu kwa kuzingatia faidi zake, kwetu sisi tutaendelea kuwapa ushirikiano na siku hizi TUCTA hatugongi meza bali tunakuja na hoja zetu mezani,” alisema Nyamhokya.

Awali akieleza historia ya uwepo wa bodi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa WCF aliwataja Wajumbe wapya wa Bodi walioteuliwa na Mhe. Waziri Jenista Mhagama ni pamoja na Ornorius John Njole, Perfect Raphael Kilenzi, Ibrahim Barnabas Mahuni, Abdulaziz Alladin Shambe, Rifai A. Mkumba, Julian C.N. Mpanduji,Raymond Kaseko, Rehema Rashid Ludanga na Felix Kagisa Rugarabamu.

=MWISHO=